Miaka 25 ya Jukwaa la Watu wa Asili Tanzania imepiga hatua kutujumuisha: Ole Kulet Mwarabu
Haki ya afya kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa ni haki ya kila mtu bila kujali uko kwenye kundi au jamii gani. Huo ulikuwa ni msisitizo mwaka huu kwenye Jukwaa la jamii za watu wa asili lililokuja jamvi wiki iliyopita hapa New York Marekani. Na kandoni mwa kikao hicho Flora Nducha alipata fursa ya kuzungumza na mshiriki kutoka Tanzania kwenye jamii ya Wamaasai mwana harakati wa haki za jamii hiyo Adam Kulet Ole Mwarabu aliyeanza kwa kumueleza kwanini mwaka huu ni wa kipekee kwa watu wa jamii za asili.
Katika ukumbi wa Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani, viongozi, watu kutoka jamii za asili na wadau mbalmbali kutoka pembe mbalimbali za dunia walikusanyika wiki iliyopita kuadhimisha miaka 25 ya Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wa Asili.
Miongoni mwa washiriki hao alikuwa Adan Ole Kulet Mwarabu, mwanaharakati wa haki za watu wa jamii za asili kutoka jamii ya Wamaasai nchini Tanzania, ambaye amesema safari ya robo karne ya jukwaa hilo imeleta mafanikio makubwa katika kutambua na kutetea haki za watu wa asili duniani.
“Kwanza tunasherehekea miaka ishirini na tano ya kuanzishwa kwa jukwaa la Umoja wa Mataifa wa watu wa asili,” amesema Adan Ole Kulet Mwarabu katika mahojiano na Flora Nducha wa Idhaa ya Kiswahili ya Umoja wa Mataifa. “Ni safari kubwa na ndefu kutoka Geneva hadi hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa New York.”
Kutoka kutotambuliwa hadi kuwa na sauti duniani
Kwa mujibu wa mwanaharakati huyo, moja ya mafanikio makubwa ya jukwaa hilo ni utambuzi rasmi wa haki za watu wa asili ndani ya mfumo wa kimataifa.
Amekumbusha historia ya makabila ya wenyeji wa Marekani waliowahi kugonga milango ya taasisi za kimataifa kutafuta sauti na kutambuliwa, kabla ya kuanzishwa rasmi kwa Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa mwaka 2002.
“Kilikuwa ni kipindi kigumu sana kwa watu wa asili kupata nafasi ya kusikilizwa,” amesema. “Lakini sasa kila mwaka tunapata nafasi ya kuwasilisha changamoto za maendeleo katika maeneo yetu na kuishauri dunia namna ya kuhakikisha watu wa asili wanaishi maisha sawa na wengine.”
Kwa mujibu wake, jukwaa hilo limekuwa sehemu muhimu ya kubadilishana uzoefu, kujifunza sera nzuri kutoka mataifa mengine na kuimarisha ushiriki wa kisiasa kwa jamii za asili.
“Tunapata nafasi ya kutetea nafasi ya kusikilizwa, lakini pia kujifunza yale mazuri yanayofanywa na nchi nyingine ili tuyatumie katika nchi zetu,” amesema.
Tanzania yatambulika kwa hatua za ushirikishwaji
Akizungumzia hali ya Tanzania, Adam Ole Kulet amesema nchi imepiga hatua kubwa tangu kupitishwa kwa Azimio la Umoja wa Mataifa la Haki za Watu wa Asili mwaka 2007, ambapo Tanzania ilikuwa miongoni mwa nchi zilizoliunga mkono.
“Ni mafanikio makubwa,” amesema kwa msisitizo. “Tanzania imeweza kutoa nafasi kwa watu wa asili kushiriki katika michakato ya maendeleo tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.”
Ametaja miradi mbalimbali mikubwa ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa mfumo wa mabasi yaendayo kasi Dar es Salaam pamoja na mradi wa bomba la mafuta kutoka Uganda hadi Bandari ya Tanga, ambapo amesema jamii za asili zimepewa nafasi ya kutoa maoni yao.
“Sauti yao haikuweza kusikilizwa zamani,” amesema. “Lakini sasa kuna hatua kubwa imepigwa katika kuhakikisha ushirikishwaji.”
Aidha amesema hata katika miradi ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, jamii za asili zimeanza kushirikishwa katika maamuzi yanayogusa maisha yao.
Maarifa ya jadi na changamoto za huduma za afya
Mwaka huu, Jukwaa la Kudumu la Umoja wa Mataifa kuhusu Watu wa Asili lilielekeza mjadala wake katika haki ya afya kwa jamii za asili.
Kwa upande wa Tanzania, Adam Ole Kulet amesema bado jamii za asili zina mchango mkubwa kupitia maarifa ya tiba za jadi ambazo zimeendelea kusaidia jamii nyingi, hasa wakati wa janga la coronavirus">COVID-19.
“Wakati wa korona tuliweza kutumia dawa za asili kujifukiza,” amesema. “Kuna maarifa ya asili ambayo yanaweza kuhifadhiwa kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo.”
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto kwa jamii zinazofuata mfumo wa maisha wa kuhamahama, hali inayofanya upatikanaji wa huduma za afya na elimu kuwa mgumu.
“Changamoto kubwa ni mfumo wetu wa kuhamahama,” ameeleza. “Huduma zinapaswa kuendana na maisha ya watu wa asili. Tukihama upande mwingine, huduma nazo zinapaswa kutufikia huko.”
Pia amesisitiza umuhimu wa kuboresha miundombinu kama barabara ili kurahisisha upatikanaji wa huduma muhimu kwa jamii hizo.
Ni mafanikio makubwa duniani
Licha ya changamoto zilizopo, Adam Ole Kulet anaamini kuwa miaka 25 ya jukwaa hilo ni ushahidi wa mafanikio makubwa katika harakati za haki za watu wa jamii za asili duniani.
“Kwa ujumla ni mafanikio makubwa duniani,” amesema. “Watu wa asili wanapokutana hapa, tunapata nguvu ya pamoja ya kutetea haki zetu na kuhakikisha sauti zetu zinasikika.”
Kauli yake inaakisi matumaini ya maelfu ya jamii za watu wa asili duniani ambazo zinaendelea kupigania haki ya kutambuliwa, kushirikishwa na kuheshimiwa katika maendeleo ya dunia ya sasa.