“Kwa sasa tunapanda aina tofauti za kunde na maharagwe katika ardhi hii ikiwa ni mara ya kwanza baada ya miaka mingi,” anasema Germathes Charles, ambaye kama walivyo wanajamii wengine alilipwa na WFP kushiriki katika kazi ya ufufuaji wa ardhi hiyo.
Katika maeneo ya mabondeni mwa Paul Atrel mafuriko yamekuwa yakitokea mara kwa mara, na kusababisha athari ikiwemo kubadili maisha ya watu. Shule hii ya msingi katika eneo la Cabaret ilifungwa baada ya mafuriko na wanafunzi walilazimika kusaka shule nyingine kuweza kuendelea na elimu.
“Mvua inaponyesha huwa tunategemea zahma” anasema Rose Marie Fleurinord. “Siku moja mvua iliponyesha nilikimbia kwenda kumsaidia Jirani yangu ambaye nyumba yake ilifurika na jamii nzima ilikuja kunisaidia, lakini nilipoteza kila kitu. Kama jamii tulifahamu nini cha kufanya kuzuia mafuriko , lakini hatukuwa na fedha za kuweza kufanya hivyo.”
Suluhu ilikuwa ni kujenga majengo ambayo yatadhibiti mtoiririko wa maji na kuzuia mafuriko. WFP ilisidia kazi hiyo kama sehemu ya program yake ya msaada wa chakula kwa ajili ya mali. Mfanyakazi wa WFP Rose Senoviala Desir, anasema shule na nyumba hivi sasa zinalindwa vizuri akiongeza kwamba “Hivi sasa watu wanaweza kulima mazao katika ardhi ambazo zilikuwa zinafurika kila mara siku za nyuma.”
Maili chache tu kutoka hapa milimani katika Kijiji cha Troissel, jamii ilifanyakazi kwa msaada wa wizara ya kazi ya nchi hiyo (MTPTC) na WFP kujenga barabara ambayo imewaunganisha kwa mara ya kwanza na masoko katika eneo hilo, vituo vya afya na shule.
“Sote tulifanyakazi na tulilipwa kwa kutoa mawe barabarani lakini pia kwa kuchimba ili kujenga barabara” anasema Jean Ronel Saint-Preux. Familia hivi sasa zinaweza kusafiri kwenda kuuza bidhaa sokoni kwa kutumia dakika 40 kwa bodaboda kwenda na kurudi badala ya saa saba tulizokuwa tukitumia kwenda kwa mguu siku za nyuma.Wengi wameweka akiba katika benki ya jumuiya iliyoanzishwa kama sehemu ya mradi wa ukarabati wa barabara.