
2. Wanazungumza lugha nyingi za Dunia
Lugha za asili zina mifumo mipana na migumu ya maarifa, ni nguzo muhimu ya utambulisho wa watu wa asili fulani, na uhifadhi wa tamaduni zao, maono yao kwa ulimwengu na pia namna ya kutoa maoni binafsi.
Takriban lugha 40 kati ya lugha 7,000 zipo hatarini kupotea. Inakadiriwa kuwa kila lugha moja ya asili inapotea kila baada ya wiki mbili. Mwaka ujao wa 2022, Umoja wa Mataifa utaanza hatua muhimu ya muongo wa lugha za asili (2022-2032).

3. Wapo kwenye kundi la watu masikini na wanaoteseka
Zaidi ya asilimia 86 ya watu wa jamii za asili wanajishughulisha na kazi zisizo rasmi na wapo kwenye uwezekano mara tatu zaidi kuishi katika ufukara. Watu hawa wana uwezekano mkubwa wa kuugua utapiamlo, na kukosa ulinzi wa kutosha wa kijamii na rasilimali za kiuchumi .

4. Hawaishi muda mrefu na kiwango cha elimu ni kidogo
Muda wa kuishi duniani kwa watu wa jamii ya asili ni mfupi kwa miaka 20 ikilinganishwa na jamii nyinginezo. Watu hawa mara nyingi hukosa huduma muhimu za afya na taarifa, pia wana uwezekano mkubwa wa kupata magonjwa kama malaria, kifua kikuu na UKIMWI.
Asilimia 47 ya watu wa asili walioko kwenye ajira hawana elimu rasmi, na kwa upande wa wanawake asilimia ni kubwa zaidi.

5. Wanawake wa jamii ya asili wana uwezekano mkubwa wa kubaguliwa na kunyanyaswa
Wanawake wa jamii za asili wana uwezekano mkubwa wa kuteswa, ubaguzi na ukatili. Takwimu zinaonesha zaidi ya mwanamke mmoja kati ya watatu wamenyanyaswa kijinsia. Pia viwango vya vifo vya wajawazito, mimba za utotoni na magonjwa ya zinaa vipo juu.
Azimio la haki za watu wa asili limetaja mahitaji yao na haki zao na limetaka hatua zichukuliwe ili kuwalinda dhidi ya unyanyasaji

6. Wengi hawana haki ya kumiliki ardhi zao
Ingawa watu wengi wa asili wanajitawala wenyewe, lakini bado wako chini ya mamlaka kuu za serikali kuu ambazo ndio zinazodhibiti ardhi na rasilimali zao. Pamoja na hayo watu wa jamii za asili sehemu mbalimbali wameonesha utawala bora zaidi duniani.

7. Wanaongoza kwenye uhifadhi wa mazingira
Watu wa jamii ya asili ni warithi na wanatekeleza upekee wa tamaduni na njia za maisha. Takriban watu milioni 70 maisha yao hutegemea misitu, na wengi zaidi ni wakulima, wafugaji na wawindaji.
Jamii hizi hustawi kwa kuishi kwa amani na mazingira yao. Utafiti unaonesha maeneo ya vikundi vya watu wa asili kuna usimamizi mzuri wa ardhi, misitu na bioanuai hustawi.

8. Wanapambana na mabadiliko ya tabianchi kila siku
Mchango wa watu wa asili katika kupambana na mabadiliko ya hali ya hewa ni mkubwa zaidi kuliko ilivyofikiriwa hapo awali. Misitu yao hufyonza angalau robo ya kaboni ya misitu ya kitropiki kwa takriban tani trilioni 55. Hii ni sawa na mara nne zaidi ya jumla ya uzalishaji wa kaboni kwa mwaka 2014.
Hakuna takwimu zilizopatika katika maeneo yote wanamoishi jamii za asili ulimwenguni, hata hivyo mchango wao ni mkubwa zaidi.

9. Ni nguzo muhimu kwa ajenda 2030 ya malengo ya maendeleo endelevu SDGs
Watu hawa wanajishughulisha moja kwa moja kuanzia kulinda mazingira na kushughulikia usawa, kuhakikisha amani na usalama, kwa ujumla Malengo ya Maendeleo Endelevu ya Umoja wa Mataifa SDGs hayatafikiwa bila watu hawa wa asili.
Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa umezitaka nchi kusisitiza haki zao wakati wa kutekeleza ajenda ya 2030.

10. Tamko la UN halitafikiwa bila ya msaada wa watu wote ulimwenguni
Azimio la Umoja wa Mataifa juu ya haki za watu wa asili ni hatua muhimu katika mshikamano na Wazawa na jamii ya ulimwengu. Lakini, kuna mapungufu makubwa kati ya utambuzi rasmi wa haki za asili na ukweli.
Tangu kupitishwa kwake mwaka 2007, nchi kadhaa, haswa Amerika Kusini, zimechukua hatua za kutambua utambulisho na haki za watu wa asili, lakini kuna mengi zaidi ya kufanya.