
Mtoto ana haki ya kucheza! Ingawa watoto hawa nchini Chad ni wakimbizi, bado UNICEF imewajengea mazingira rafiki waweze kukutana na kucheza na kufurahia maisha yao.Michezo ni muhimu kwa kuimarisha viungo na kujenga fursa ya mtoto kupanua uwezo wa kufikiria.

Uwepo wa huduma ya choo shuleni ni moja ya tiketi ya kuwezesha watoto wote hasa wa kike kwenda shuleni wanapokuwa kwenye hedhi. Huko Sudan Kusini, UNICEF imejenga matundu ya vyoo katika shule, matundu ambayo yana mshikio wa kumwezesha hata mtoto mwenye ulemavu kutumia huduma hii.

Mazingira hatarishi husababisha watoto hasa wa kike kupata ujauzito na kuacha masomo. Pichani binti huyu mwenye umri wa miaka 14 alipata ujauzito na hapa amebeba mwanae. Alilazimishwa kuolewa lakini baada ya wahudumu wa kijamii kuingilia kati, ndoa ilivyunjwa na sasa amerejea kwa wazazi wake Kasese nchini Uganda na anajiandaa kurejea kupitia mradi wa UNICEF wa kusaidia vijana barubaru na vijana balehe nchini Uganda.

Tukirejea nchini Chad, ukimbizi usiwe sababu ya mtoto kukosa haki yake ya msingi ya kuendelezwa kwa kupatiwa elimu. UNICEF na wadau wanatekeleza mkataba wa kimataifa wa haki za mtoto CRC pamoja na ajenda ya Afrika 2040 ya kuweka mazingira sahihi ikiwemo shule ili mtoto wa Afrika kukuza ustawi wake.

Kuna na ulemavu wa viungo siyo kikwazo cha mtoto kwenda shuleni. Nchini Cameroon mtoto huyu
Moustapha Modou akiwa shuleni na vifaa vya shuleni alivyopatiwa na UNICEF na shule hii ni jumuishi ikileta watoto wote pamoja wakiwemo wasio na ulemavu na wenye ulemavu kama vile mtindio wa ubongo, viziwi, na wenye ulemavu wa viungo.

Majanga ya asili hayatabiriki. Baba na wanae huko Goma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC walilazimika kukimbia baada ya volkano katika mlima Nyiragongo jimboni Kivu Kaskazini kulipuka tarehe 22 mwezi Mei mwaka huu. UNICEF inahaha kuwapatia mazingira salama ili watoto waendelee kupata haki zao za kuishi, kuendelezwa, kulindwa na kushirikishwa.