
Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula (WFP), limetunukiwa tuzo ya amani ya Nobel ya mwaka 2020. Kamati ya Nobel imesema WFP imetambuliwa “kwa juhudi zake za kupambana na njaa, kwa mchango wake wa kuboresha mazingira kwa ajili ya amani katika maeneo yaliyoathirika na vita na kwa kuwa chachu katika kuzuia matumizi ya njaa kama silaha ya vita na migogoro”.

Kamati ya Nobel imesema janga la COVID-19 litaongeza njaa na kuwaacha watu milioni 265 wakikabiliwa na njaa kubwa ndani ya mwaka mmoja. WFP imesema itatumia uzoefu wake katika hatua za dharura na masuala ya kiufundi na mnyororo wa usambazaji kuwafikia kuwafikia watu wengi zaidi na msaada kadri inavyowezekana.

Akishukuru kuhusu tuzo hiyo mkurugenzi mtendaji wa WFP, David Beasley, amesema “shirika hilo limepokea tuzo kwa unyenyekevu mkubwa" akiongeza kwamba “Palipo na vita pana njaa, na palipo na njaa mara nyingi kuna vita. Leo ni kumbusho kwamba uhakika wa chakula, amani na utulivu vinakwenda sanjari. Bila amani hatuwezi kufikia lengo la kimataifa la kutokomeza njaa.”

Bwana. Beasley amewapongeza wafanyakazi wa WFP kwa kazi yao inayochagizwa na “Maadili yetu ya pamoja ya uadilifu, utu na ujumuishaji”, na kuongeza kwamba." “Tuzo ya amani ya Nobel sio kwa WFP peke yake” ni kutambua umuhimu wa ushirikiano na serikali, mashirika na wadau wa sekta binafsi.

Likiwa limeanzishwa mwaka 1961 shirika hilo la WFP linajitaja kama “shirika kubwa zaidi duniani la msaada wa kibinadamu" linaokoa maisha katika hali za dharura, kuleta mafanikio na kusaidia mustakabali endelevu kwa watu wanaojikwamua kutoka kwenye vita, majanga na athari za mbadiliko ya tabianchi.”