
Suzan Kiden ni mteguaji wa mabomu wa UNMAS tangu mwaka 2015. Kutana na Suzan Kiden yeye ni mteguaji mabomu wa UNMAS tangu mwaka 2015. Anasema “nilifundishwa kazi hii ili kuokoa maisha ya watu wangu wa Sudan Kusini. Ninaipenda kazi yangu. Kinachonifurahisha zaidi ni kuondoa tishio la mabomu ya ardhini. Tukisaidia kuondoa mabomu, tutaweza kulima na kuanzisha mahala pa kukaa, huku tukiwasaidia watu kutembea kwa uhuru bila uwoga maana mabomu yanaweza kuua watu bila ubaguzi. Kwa kweli nilifanya kazi hii bila ubaguzi wowote, nilifanya kazi sawa na wafanyakazi wa kiume. “

Tarehe 29 mwezi Septemba mwaka huu, UNMAS ilifanya operesheni ya kuharibu tani 1.2 za vilipuzi vilivyosalia baada ya vita. Vilipuzi hivi vilibainika wakati wa operesheni za kukagua na kusafisha eneo la makazi ya raia pamoja na mashamba huko Juba, eneo ambalo ni karibu pia na makao makuu ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa huko Sudan Kusini, UNMISS

Tarehe 28 mwezi Septemba mwaka huu, UNMAS iliteketeza takribani silaha ndogo ndogo 15,000 ambazo zilibainika kwenye makazi ya wenyeji pamoja na mashambani huko Juba. Silaha hizi zilibainika wakati wa msako maalum ulioendeshwa kwa wiki chache. Silaha hizi ndogo ndogo zimekuwa kichocheo kikubwa cha mapigano ya wenyewe kwa wenyewe huko Sudan Kusini.

Rebecca Morris na mwanae wakiwa mbele ya makazi yao yaitwayo Tukul. Pichani Rebecca anazungumza na Andrew Deng ambaye ni afisa uhusiano wa jamii. Alirejea hivi karibuni na mama yake na mwanae baada ya baba yake kuuawa wakati wa mgogoro mwezi Julai mwaka huu. Rebecca ameumizwa sana na kifo cha baba yake kwa sababu alikuwa akimsaidia kwenda shule lakini sasa ni vigumu kuendelea bila msaada wake. Anajisikia yuko salama baada ya kuona kazi za wateguaji mabomu ambayo inasaidia kusafisha na kuweka mazingira salama ya kurejea nyumbani.