Nchi wanachama wanaweza kuandaa mikutano kuhusu masuala muhimu ya kimataifa. Rais wa Marekani Donald Trump alizindua wito wa kuchukua hatua dhidi ya ukuaji wa matumizi ya dawa haramu duniani kote kwa kuangazia tatizo la uraibu.
Eneo la katikati mwa New York ambako ndipo makao makuu ya Umoja wa Mataifa yalipo, njia zake nyingi zimefungwa kupisha wiki ya mikutano ya ngazi ya juu. Watu wengine hawaruhusiwi kupita mitaa hii isipokuwa wanaohusika.
Katika maeneo ya Umoja wa Mataifa, sanamu la Nelson Mandela, aliyekuwa mfungwa wa kisiasa, rais wa Afrika Kusini na kiongozi wa harakati za kupambana na ubaguzi wa rangi limezinduliwa jumatatu asubuhi. Sanamu hilo ni zawadi kutoka Afrika Kusini.
Wiki hii siyo ya mfululizo wa mikutano ya ngazi ya juu tu. Jumapili ya tarehe 23 mwezi huu wa Septemba wanamuziki wawili kutoka Mali waliburudisha katika makaribisho ya wahamasishaji wa malengo ya maendeleo endelevu.
Muziki kutoka kwa watoto ulisindikiza maadhimisho ya siku ya kimataifa ya amani iliyoadhimishwa kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa Ijumaa ya tarehe 21 Septemba.
Nchi zote 193 wanachama wa Umoja wa Mataifa, zina haki ya kuongea katika mjadala mkuu kwenye ukumbi wa Baraza kuu. Kiutamaduni Brazil ndiyo huanza jumanne asubuhi, na kiongozi wa mwisho hupanda jukwaani au kusimama kwenye mimbali jumatatu inayofuata.