Shatha, mwenye umri wa miaka 26, ana shahada ya uuguzi na ni mama wa watoto wawili. Aliweza kukamilisha masomo yake wakati wa vita, akijifunza kwa vitendo hospitalini huku akifanya kazi. Anasema "Kuwaacha watoto wangu na kuja hospitalini kusoma ilikuwa vigumu wakati wa vita. Ninapofanya kazi, mimi huwapa wagonjwa msaada wa kihisia, si matibabu tu.”
Shatha anatarajia kukamilisha shahada ya uzamili ili kuendelea kujifunza na kutoa huduma muhimu.
Noor, mwenye umri wa miaka 26, ni daktari katika idara ya mapafu. Wakati wa vita alihama hadi kusini mwa Gaza na alipitia kipindi kigumu kuwa mbali na familia yake.
Anasema “Fursa hii imeboresha taaluma yangu, nina wahudumia wagonjwa 25 kila siku, na wakati mwingine zaidi. Ninafanya kazi kama daktari wa jumla, mara nyingi nikiona wagonjwa wenye pumu na magonjwa ya kuambukiza ya mapafu. Vita vilifanya maisha kuwa magumu kwa watu, kuni ndio zilitumika kama mbadala ya gesi na hii imeongeza magonjwa ya kupumua. Pia kuna maambukizi zaidi ya virusi kutokana na msongamano na hali ngumu ya maisha katika mahema.”
Hamza, mwenye umri wa miaka 30, alikamilisha masomo yake nchini Sudan mwaka wa 2022 na wakati wa vita alikuwa akifanya kazi katika idara ya upasuaji wa neva. Anasema “Tumeona wgonjwa wengi, wengine ilikuwa vigumu kuwapatia matibabu hasa wale waliopata majeraha makubwa ya kichwa. Vita vilichukua kila kitu kwetu na tunajaribu kuunda mwanzo mpya na kuleta mabadiliko.”
Hamza, ambaye sasa ni daktari wa kawaida, anamipango ya kuwa daktari bingwa wa upasuaji wa neva.
Mohammed, mwenye umri wa miaka 31, alikamilisha masomo yake katika Chuo Kikuu cha Kiislamu na anafanya kazi katika idara ya dharura. Mwaka 2024, alipokuwa akifanya kazi kama daktari, alipigwa risasi na mifupa miwili kwenye mguu wake ikavunjika. Akiwa amepona jeraha, yeye mwenyewe ni mfano wa jinsi kupona si dhana ya siku zijazo bali kunatokea sasa kupitia huduma, ustahimilivu na fursa.
Anasema “Tunapokea wagonjwa wa kila aina katika idara ya dharura, sasa tunaona wagonjwa wengi wenye shinikizo la damu na maambukizi. Fursa hii (ya ajira kutoka UNDP) inanisaidia kujenga upya maisha yangu na kusaidia matibabu yangu. Natumai nitapona haraka ili niweze kufanya kazi kwa ufanisi. Kutembea kwangu kumeimarika lakini bado ninahitaji muda zaidi wa kupona kikamilifu.”
Tamer, mwenye umri wa miaka 28, alikamilisha masomo yake nchini Misri na ni daktari wa jumla. Anasema “Mwanzoni mwa vita, familia yangu ilikuwa miongoni mwa watu wa kwanza kuhamishwa kuelekea kusini mwa Gaza. Kisha, nilitumia miezi 17 kujitolea katika idara ya dharura. Ilikuwa vigumu kuwaona watu wote waliohitaji huduma ya haraka wakati tulikosa vifaa vya matibabu.”
Tamer amejitolea kupanua ujuzi wake na kutafuta utaalamu wa matibabu. Anasema “Kwa mkataba huu mpya, (kutoka UNDP) nilianza upya katika idara ya upasuaji wa neva. Ninapanga kuomba mtihani wa uteuzi mwezi ujao na kipaumbele changu cha kwanza ni kuwa daktari wa upasuaji wa neva.”