Kaunti ya Samburu kaskazini mwa Kenya ni miongoni mwa kaunti kubwa zaidi nchini na yenye idadi ndogo ya watu. Vituo vya afya vimetawanyika kwa umbali mkubwa, wakati mwingine zaidi ya kilomita 50 kutoka kituo kimoja hadi kingine. Sasa huduma tembezi za afya zinatolewa kwa kutumia magari.
Kliniki tembezi hutoa huduma za uzazi wa mpango, huduma baada ya utoaji mimba, huduma za kabla na baada ya kujifungua, uchunguzi wa saratani ya sihngo ya kizazi na titi, uchunguzi na matibabu ya maambukizi ya magonjwa ya zinaa, tathmini ya lishe, msaada wa dharura za uzazi, pamoja na huduma kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.
“Nimemleta binti yangu kwa uchunguzi wa afya. Amepokea virutubisho vya lishe na maziwa ya tiba ili kusaidia ukuaji wake,” anasema Namano Lekashira. “Nikiwa hapa, pia ninasubiri kufanyiwa uchunguzi wa saratani ya shingo ya kizazi na titi. Uwezo wa kupata huduma kwa ajili yetu sote katika ziara moja ni msaada mkubwa sana.”
Ni asilimia 27 pekee ya wanawake walioolewa katika kaunti hiyo wanaotumia njia za kisasa za uzazi wa mpango, kiwango kilicho chini ya wastani wa kitaifa wa asilimia 57. Kitaifa, takribani asilimia 53 ya mahitaji ya uzazi wa mpango yanatimizwa, jambo linaloonesha kuwa takribani nusu ya wanawake wanaotaka kupanga au kuzuia mimba hawapati huduma zinazofaa.
Kila kituo kilihudumiwa na wataalamu wa afya 11, wakiwemo wauguzi, maafisa wa kliniki, wataalamu wa lishe, wahamasishaji wa afya ya jamii na wataalamu wa maabara. Kwa jumla, wananchi 4,600 kutoka jamii za wafugaji zilizo vigumu kufikika na makazi yasiyo rasmi walipatiwa huduma.