Leo ni siku ya kipekee watoto wanatabasamu baada ya kupokea vifaa vya kujifunzia — mabegi ya shule, penseli, daftari, vifutio, rangi za kuchorea, rula, na vifaa vya hisabati.
Shule hii ya wasichana ya Arabee Aradawiya imejaa. Wasichana wanakimbia, wanacheza, wanashirikiana kwa utani na wakikula vitafunwa, na kunong’onezana kabla ya kengele kupigwa. Madarasa yamejaa wanafunzi wanne kwa benchi moja, walimu wawili kwa somo.
Shule si tu kwamba zinaendeleza elimu kwa mamilioni ya watoto nchini Sudan, bali pia zinatoa maeneo salama wakati wa vita vinavyoendelea. “Kampeni hii ni muhimu sana kwa sababu inawawezesha watoto kuendelea kujifunza baada ya zaidi ya miaka miwili ya kukosa shule. Huo ni upotevu mkubwa wa elimu,” anasema Abdalla Dagot, Afisa Elimu wa UNICEF. Shule hii ni mojawapo ya mamia ya shule za msingi katika jimbo hili zinazofikiwa chini ya mpango wa Muungano wa Ulaya wa Kujumuisha na Kuwaunganisha Watoto Wakimbizi Katika Mfumo wa Elimu wa Sudan (IRCSES). Watoto zaidi katika majimbo ya River Nile na Kassala pia watanufaika kupitia mpango huu. “Mtoto asiye na penseli hana mustakabali,” anaongeza.
Anfal, Msichana mwenye umri wa miaka 10 ni mwanafunzi katika shule ya wasichana ya Arabee Aradawiya huko Damazine, Jimbo la Blue Nile. Anasema “Elimu ni muhimu sana kwetu. Lazima tuende shule hata wakati wa vita ili tuweze kujifunza.” Idadi ya wanafunzi sasa imefikia 500, ikiwa ni pamoja na watoto 120 waliopoteza makazi na wakimbizi.
Walaa, mwanafunzi wa darasa la tatu katika shule ya wasichana ya Arabee Aradawiya anasema alitamani sana kurudi shule sana. “Kitu ninachopenda zaidi ni rangi na madaftari,” anasema.
Kwa kuongozwa na kauli mbiu ya kutomwacha mtoto yeyote nyuma, mpango huu utatoa elimu salama, jumuishi na yenye ubora kwa watoto zaidi ya 170,100 katika shule zote 418 za Jimbo la Blue Nile — wakiwemo watoto waliopoteza makazi, wakimbizi na watoto wa jamii zinazowapokea.
Aden ni msichana mwenye umri wa miaka 10. Hapa ameshikilia kifaa chake kipya cha hisabati, akiwa na matarajio ya kuimarika katika somo lake analolipenda zaidi - hisabati.
“Hakuna muda wa kuacha masomo. Elimu itatusaidia kujenga upya nchi yetu.” anasema.
Wengi wa watoto Sudan waliacha kila kitu nyuma walipolazimika kukimbia mzozo, na familia haziwezi kumudu hata mahitaji ya kimsingi.
Renad amefurahi kupokea begi linalohifadhi vizuri vifaa vyake vya elimu. Hapo awali alitumia mfuko wa plastiki kubeba vitabu na kalamu yake. Sasa, akiwa na begi lake jipya, madaftari yake yako salama na yamepangwa vizuri. Kwake, kurudi shuleni kunamaanisha muda zaidi na matembezi ya asubuhi ya thamani pamoja na marafiki.
Kama sehemu ya kampeni hii, UNICEF inawapatia mashule pia vifaa vya walimu - rula, vipimo vya dira, chaki, saa za kufundishia, na daftari ili kuboresha utoaji wa masomo na ujifunzaji kwa watoto waliopoteza makazi na wale walio katika mazingira magumu.
Mkuu wa shule Noor Abdalrahman ameishukuru UNICEF kwa msaada wa wakati muafaka huku akielezea mahitaji makubwa yaliyopo.