UNICEF/Michael Songa | Kwenye machimbo ya mawe katika jamii ya Gombu huko Kenema, Sierra Leone, Adama (kulia, akiwa amevaa gauni jeusi lenye madoa meupe), mwenye umri wa miaka 12, pamoja na marafiki zake hufanya kazi pamoja na watu wazima, wakivunja vipande vikubwa vya granite kuwa kokoto kwa ajili ya kuwauzia wakandarasi wa ujenzi.
Ojulu Omod, mvulana mwenye umri wa miaka 13 nchini Ethiopia, hayuko shuleni. Badala yake anaiunga mkono familia yake kwa kuchimba dhahabu kwa njia ya kijadi kusaidia kipato.
Kutana na Safari, mtoto mwenye umri wa miaka 14, akiponda kokoto kwenye machimbo ya mawe ya Kalehe, jimboni Kivu Kusini, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Ayiwane Aconga kutoka Ethiopia, akitosa nyavu mtoni kujipatia samaki. Aliacha shule darasa la 5 baada ya kufurushwa na mzozo. Sasa anaishi na shangazi yake ambaye hujipatia riziki kwa kuuza samaki sokoni mtaani kwao.
Kutana na mtoto huyu anayeishi na kufanya kazi mitaani ya kuuza maua na vifaa vya nyumbani ili kujipatia riziki katika mitaa yenye msongamano wa watu huko Dhaka, Bangladesh.
Hapa nchini Mali katika jimbo la Kayes, mtoto wa kike anatumia kibuyu kusaka dhahabu. Nchini Mali, watoto wengi wananyimwa haki zao za msingi za afya na elimu kwa kufanya kazi kwenye migodi ya dhahabu.
Si chaguo lake kuuza ndizi mtaani bali ni umaskini umemsukuma Rafiqullah, mwenye umri wa miaka 12, kuuza ndizi Tarinkot, mji mkuu wa jimbo la Uruzgan nchini Afghanistan.