
Miezi ya mapigano huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imewalazimu mamia ya maelfu ya watu kukimbia makazi yao. Maelfu kati yao wanatafuta usalama katika nchi jirani. Kadri ghasia na uhamishaji wa watu vinavyozidi kuongezeka, Burundi na Uganda zimekuwa kimbilio salama kwa maelfu ya wakimbizi kutoka DRC. Burundi imepokea idadi kubwa zaidi ya wakimbizi, na kwa kushirikiana na mamlaka za Burundi pamoja na washirika wa kibinadamu, WFP inatoa msaada wa chakula wa kuokoa maisha kwa wakimbizi hao.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) inakabiliwa na janga kubwa la njaa duniani. Njaa inaendeleza hali hiyo, huku migogoro inayotumia silaha na uhamishaji mkubwa wa watu vikichochea zaidi tatizo hilo. WFP iliwafikia mamilioni ya watu na kuwapa msaada wa kuokoa maisha wa chakula, kifedha na huduma za lishe.

Kadri mzozo katika mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) unavyozidi kuongezeka katika miezi ya hivi karibuni, ujumbe wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa, MONUSCO, imeendelea kufanya kazi ya kuwalinda raia katika maeneo yanayodhibitiwa na kundi la waasi la M23 linaloungwa mkono na Rwanda katika jimbo la Kivu Kaskazini.

Shirika la Afya Duniani (WHO) linatoa msaada muhimu wa huduma za afya katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kwa kukabiliana na milipuko ya magonjwa na kuboresha miundombinu ya afya. Kwa kushirikiana na wadau wa ndani na wa kimataifa, WHO husambaza vifaa vya dharura vya tiba, huendesha kampeni za chanjo, na kuimarisha mfumo wa afya ili kuwafikia watu walio hatarini katika maeneo ya mbali.

Huko Kivu Kaskazini,DRC, UNICEF inatoa msaada wa chakula wa kuokoa maisha kwa familia zinazokabiliwa na njaa kali kutokana na mzozo unaoendelea na uhamishaji wa watu. Kwa kuzingatia walio hatarini zaidi, wakiwemo watoto, UNICEF inasambaza chakula muhimu ili kuhakikisha familia zinaweza kuendelea kuishi na kuanza safari ya kurejea katika hali ya kawaida.
Mbali na chakula, UNICEF pia inafanya kazi ya kuboresha upatikanaji wa maji safi, huduma za afya, na elimu, ikishughulikia mahitaji ya jumla ya jamii zilizo katika mgogoro.


Huko Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, upatikanaji wa huduma za afya ya uzazi ulikuwa hafifu na hivyo kuna viwango vya juu zaidi vya vifo vya kina mama. UNFPA imepeleka wakunga zaidi na wahudumu wa jamii kote Goma ili kuhakikisha huduma zinaendelea kutolewa bila kusitishwa na kupunguza vifo vya kina mama na watoto wachanga.

UNFPA hutoa huduma muhimu za kibinadamu nchini DRC, ikilenga afya ya uzazi na afya ya kijinsia kwa wanawake na wasichana. Katika mazingira ya migogoro na uhamishaji wa watu, UNFPA inatoa huduma za afya ya uzazi , vifaa vya afya ya uzazi, na msaada kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia.