
Hatimaye baada ya mafunzo, vijana wameweza kulima mboga kwa mfumo waliofundishwa na walinda amani wa Umoja wa Mataifa kutoka Thailand wanaohudumu nchini Sudan. Bustani za aina hii pamoja na kutumia eneo dogo, zinaepusha usumbufu wa udongo na pia kuepusha utupaji holela wa chupa za plastiki. Na zaidi ya yote vijana wanajipatia sio tu mboga lakini pia wanauza na kupata kipato na hivyo kuepuka kutumikishwa vitani.

Huduma ya afya inatolewa na walinda amani wa UN kutoka Senegal wanaohudumu nchini Mali kupitia MINUSMA. Hapa ni Mopti, katikati ya Mali. Huduma za uchunguzi wa afya ziliambatana pia na uhamasishaji wa jamii na elimu kuhusu kuishi kwa utangamano, haki za binadamu, sheria sambamba na mgao wa vifaa kwa jamii.

Kuelekea uchaguzi mdogo nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, CAR mwezi Julai mwaka 2023, walinda amani wa UN kutoka Burundi wanaohudumu ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo MINUSCA wanaelimisha jamii ya Boubou jinsi ya kukabiliana na kauli za chuki.,

Hapa ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC na kulia ni Mshauri wa Jinsia wa ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini humo, MONUSCO, Meja Rachel Grimes akizungumza na wanawake zaidi ya 50 wa eneo la Eringeti jimboni Kivu Kaskazini kupata maoni yao baada ya waasi kuwashambulia. Wanawake wanataka ulinzi uimarishwe ili waweze kuendelea na shughuli zao ikiwemo kilimo.

Guetel Moiba Esther Adrienne, (pichani) akiwakilisha kundi lililojihami nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati, (CAR) akitia saini makubaliano ya kisiasa ya amani na maridhiano ya mwaka 2019 yaliyofanyika nchini Sudan. ilikuwa mara ya kwanza wanawake kwa wanne kushiriki kwenye mazungumzo ya amani.