Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNGA80

Mkutano wa Baraza Kuu - Taarifa Maalum ya UNGA80
23 Septemba – 30 Septemba 2025
Jukwaa limewekwa tayari kwa ajili ya Mjadala Mkuu wa Mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.
Mkutano huu utafunguliwa chini ya kaulimbiu “Bora Pamoja: Miaka 80 na Zaidi kwa Amani, Maendeleo na Haki za Binadamu”, ikiwa ni hatua muhimu inayofanyika katikati ya changamoto kubwa duniani na wito wa dharura wa kuchukua hatua mpya za ushirikiano wa kimataifa.
Mjadala wa Ngazi ya Juu utaanza rasmi tarehe 22 Septemba kwa siku nzima ya mikutano ya kilele na maadhimisho, ikiwemo kumbukumbu ya miaka 80 tangu kuanzishwa kwa Umoja wa Mataifa, tukio la wakati wa Malengo ya Maendeleo Endelevu au SDG Moment na kutimia miaka 30 tangu Mkutano wa Dunia wa Beijing kuhusu wanawake. Viongozi pia watashiriki kwenye mkutano wa ngazi ya juu kuhusu Suluhu ya amani kwa suala la Palestina na utekelezaji wa suluhu ya mataifa mawili.
Kuanzia tarehe 23 hadi 29 Septemba, macho na masikio ya dunia yatageukia jukwaa maarufu lenye marumaru ya kijani ndani ya Ukumbi wa Baraza Kuu, ambapo marais, mawaziri wakuu na wafalme watawasilisha taarifa za kitaifa, wakibainisha dira zao kuhusu amani, maendeleo, haki za binadamu na hatua za pamoja wakati huu wa changamoto zinazoongezeka duniani.
Ajenda pia itahusisha mkutano wa kilele unaofanyika kila baada ya miaka miwili kuhusu ufadhili wa maendeleo endelevu, Mkutano wa Tabianchi, uzinduzi wa Mazungumzo ya kimataifa kuhusu Usimamizi wa Akili Mnemba AI, Hatua za dunia kuhusu magonjwa yasiyoambukiza NDCs na afya ya akili, pamoja na hali ya Waislamu Warohingya na wengine walio wachache nchini Myanmar.
Hapa, Idhaa ya Kiswahili inakupa fursa ya kuketi mstari wa mbele kushuhudia yote yanayojiri. Kupitia simu yako ya rununu au kompyuta, fuatilia Wakuu wa Nchi na Serikali wanapojadili masuala makubwa ya wakati wetu na kuelekeza dira ya taswira mpya ya Umoja wa Mataifa.
 
Tembelea majukwaa yetu ya mitandao ya kijamii: Youtube: Habari za UN X: Habari za UN
UN News/Abdelmonem Makki

Akiwa Doha, Rais wa Baraza Kuu aona watoto wa kipalestina walivyo na matumaini licha ya zahma walizopita

Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa Annalena Baerbock ametembelea wakimbizi wa kipalestina huko Doha nchini Qatar kuwajulia hali na kujionea maisha yao baada ya kuondolewa wakati wa vita kali huko Ukanda wa Gaza eneo la wapalestina linalokaliwa kimabavu na Israel na kuletwa nchini Qatar kwa ajili ya kupatiwa matibabu. Leah Mushi anatupa taswira ya ziara yake hiyo.

Audio Duration
4'6"