Ukurasa huu unaleta pamoja taarifa kuhusu muongozo kutoka kwa Shirika la afya la Umoja wa Mataifa, WHO na Umoja wa Mataifa kuhusu mlipuko wa sasa wa virusi vya corona au COVID-19, ambavyo viliripotiwa mara ya kwanza Wuhan, China mnamo Desemba 31, 2019. Tafadhali tembelea ukurasa huu kupata taarifa za kila siku. WHO inafanya kazi kwa karibu na wataalam wa kimataifa, serikali na wadau kupanua ujuzi wa kisayansi kuhusu virusi hivi vipya, kutokana na jinsi vinavyosambaa na athari zake na kutoa ushauri kwa nchi na watu, kuhusu hatua za kuchukua kwa ajili ya kulinda afya na kuzuia kuenea kwa mlipuko.
Taarifa kuhusu Virusi vya Corona
04 MACHI 2020
Elimu kwa wasichana haina maana iwapo jamii ina mtazamo hasi dhidi yao imesema ripoti ya mashirika ya Umoja wa Mataifa. Virusi vya Corona vyasababisha kuahirishwa kwa mkutano wa 64 wa CSW. Tunafanya kila tuwezalo kuwasaidia waathirika wa vita Idlib imesema WFP.
Timu ya WHO yawasili Tehran ili kuisaidia Iran kupambana na COVID-19
Timu ya wataalam wa shirika la afya duniani WHO imewasili mjini Tehran ili kuisaidia nchi ya Iran katika juhudi zinazoendelea za kupambana na mlipuko wa virusi vya Corona (COVID-19) nchini humo.
UN yatoa dola milioni 15 za kimarekani kukabiliana na COVID-19
Umoja wa Mataifa kupitia ofisi yake ya kuratibu masuala ya kibinadamu na misaada ya dharura OCHA umetoa dola milioni 15 za kimarekani kutoka katika mfuko wa dharura wa Umoja wa Mataifa CERF ili zisaidie juhudi za ulimwengu kudhibiti kusambaa kwa ugonjwa wa COVID-19, hususani katika nchi zenye mfumo duni wa huduma za afya.
Corona isituchanganye, tuchukue hatua; Syria nako ni janga linalotia shaka zaidi- Guterres
Makombora yakizidi kumiminikia raia wasio na hatia nchini Syria, huku virusi vya Corona navyo vikizidi kusambaa maeneo mbalimbali duniani, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezungumza na waandishi wa habari na kuhusu zahma hizo akisema kuwa kwa Corona huu si wakati wa kuchanganyikiwa na kwa Syria, janga hilo ni moja ya mazingira ya kutia shaka zaidi kwenye muongo wa sasa.
Mawaziri wa Afya jibuni maswali haya muone iwapo mpo tayari kudhibiti Corona
Shirika la afya ulimwenguni, WHO limeorodhesha maswali ambayo kila nchi inapaswa kujiuliza ili iweze kufahamu iwapo imejiandaa vyema kukabiliana na mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 ama la.
“Acheni unyanyapaa dhidi ya wachina na wengine wa Asia Mashariki kisa virusi vya Corona”- Bachelet
Virusi vya Corona vikiendelea kusambamba huku na kule baada ya kuripotiwa kwa mara ya kwanza nchini China, hii leo Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu, Michelle Bachelet amepaza sauti dhidi ya wale wanaotenda vitendo vya chuki na unyanyapaa dhidi ya wachina na watu wa mashariki mwa Asia.
Virusi vya Corona; nchi za Afrika Mashariki zimejiandaa- WHO
Shirika la afya ulimwenguni, WHO kanda ya Afrika Mashariki, limesema kuwa mataifa ya ukanda huo yamejiandaa kudhibiti mlipuko wa virusi vya Corona, COVID-19 wakati huu ambapo imeelezwa kwa mara ya kwanza kuna idadi kubwa ya visa vipya nje ya China.
Virusi vya Corona na utalii; UNTWO yapaza sauti
Wakati virusi vya Corona, COVID-19 vikiendelea kuibua sintofahamu duniani hivi sasa, shirika la utalii la Umoja wa Mataiaf, UNWTO limesema linashirikiana na shirika la afya ulimwenguni, WHO na wadau wengine kusaidia mataifa kutekeleza mikakati ya kupunguza rabsha zisizo za lazima katika safari na biashara za kimataifa.
WHO yataka nchi ziwasilishe taarifa kuhusu virusi vya Corona
Shirika la afya ulimwenguni, WHO limesema kuwa changamoto kubwa hivi sasa katika kudhibiti kuenea kwa virusi vya Corona, ni nchi nyingine zenye wagonjwa hao kutokuwa tayari kuwasilisha taarifa zao kwa shirika hilo.
Kila nchi lazima ifanye kila iwezalo kujiandaa dhidi ya COVID19:UN
Umoja wa Mataifa umeitaka kila nchi kote duniani kufanya kila liwezekanalo ili kujiandaa endapo mlipuko wa virusi vya Corona COVID19 utazuka.