Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA

LUGHA YA KISWAHILI KIMATAIFA
Lugha ya kiswahili kuadhimishwa kimataifa kila tarehe 7 Julai - UNESCO

Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu , sayansi na utamaduni UNESCO tarehe 23 mwezi Novemba mwaka 2021 lilitangaza rasmi tarehe 7 Julai ya kila mwaka kuwa siku ya Kiswahili duniani.

Maudhui ya maadhimisho ya mwaka huu ni Kiswahili kwa amani na ustawi. Lengo hasa la maadhimisho haya ya mwaka ni kusongesha matumizi ya lugha ya kiswahili kama nguzo ya amani, na ustawi na wakati huo kuimarisha tamaduni mbalimbali.

UNESCO ilipitisha uamuzi huo huko makao makuu yake mjini Paris Ufaransa wakati wa mkutano wa nchi wanachama wa shirika hilo.
Azimio lilipitishwa bila kupingwa na utekelezaji wake unaanza mwaka huu wa 2022.

Kupitia ukurasa huu mahsusi, utapataa taarifa zote kuanzia kupitishwa kwa azimio hilo, mapokeo yake na harakati za kukuza lugha ya Kiswahili ili iweze kujenga amani, uchumi, maendeleo na utangamano katika kona mbali mbali za dunia.

Utapata taarifa zilizochapishwa, video kutoka watu mbalimbali iwe maafisa wa serikali wa nchi wanachama wa Umoja wa Mataifa, maafisa wa UN wenyewe, wanazuoni, wanafunzi na wananchi wa kawaida.


 

Balozi Gertrude Mongella, akihojiwa na Stella VUzo wa UNIC Dar es salaam (Picha Maktaba)
UN Tanzania/Ahimidiwe Olotu

Acheni kutumia lugha msiyofahamu vyema, tumieni Kiswahili- Balozi Mongella

Miongoni mwa watu waliopokea kwa shauku kubwa kutambuliwa kwa lugha ya Kiswahili kimataifa ni aliyekuwa Rais wa Bunge la Afrika Balozi Gertrude Mongella kutoka Tanzania ambaye yeye amesema sasa anajivunia kujiita anatoka taifa linalozungumza lugha ya Kiswahili au Swahiliphone badala ya wale waingereza, Anglophone au wafaransa, Francophone.

Balozi Mongella amesema hayo katika mahojiano haya yafuatayo aliyofanya na Stella Vuzo wa Kituo cha Habari cha Umoja wa Mataifa, UNIC, jijini Dar es salaam nchini Tanzania wakati wa shamrashamra za kuelekea siku ya Kiswahili duniani tarehe 7 mwezi Julai mwaka huu.

07 JULAI 2022

Hayawi hayawi sasa yamekuwa na leo jarida linajikita katika maadhimisho ya siku ya kiswahili duniani kuanzia habari kwa ufupi ambayo imebisha hodi Paris Ufaransa kwenye makao makuu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, halikadhalika Zanzibar ambako huko Jumuiya ya Afrika MAshariki imekuwa na maadhimisho maalum bila kusahau kauli ya Gertrude Mongela kuhusu hatua ya Kiswahili kutambulika kimataifa.

Sauti
10'44"