Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

CSW70

Kamisheni ya Hali ya Wanawake Duniani
Mkutano wa 70 - CSW70

Kuanzia tarehe 9 hadi 19 Machi 2026, macho na masikio yataelekezwa katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambako kutafanyika Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70.

Hili ni jukwaa kubwa zaidi la kila mwaka la Umoja wa Mataifa linalojikita katika usawa wa kijinsia na haki za wanawake. Kinachotokea katika CSW huwa na mchango kwenye sheria, sera, ufadhili na uwajibikaji katika nchi mbalimbali na kwa vizazi tofauti.

Kinachomulikwa mwaka huu ni:  Haki, Sheria na Hatua kwa Wanawake na Wasichana wote, ikienda sambamba na kauli mbiu ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani Machi 8.

UN News

Tunatoka nje ya mahakama na kufuata wananchi kuwaelimisha – TAWJA

Upatikanaji wa haki hususan kwa wanawake na wasichana hukumbwa na vikwazo lukuki ikiwemo ukosefu wa uelewa wa haki zenyewe. Nchini Tanzania Chama cha Wanawake Majaji, (TAWJA) kimetambua pengo hilo na ndio maana tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000 kimekuwa kinachukua hatua kuhakikisha kwamba kabla ya kusaka haki, wanawake na wasichana wanatambua haki zao. Kufahamu nini kinafanyika, Assumpta Massoi wa Idhaa hii mwezi Machi mwaka huu kando ya mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani, CSW70 hapa Umoja wa Mataifa, alizungumza na Mwenyekiti wa TAWJA, Barke Sehel ambaye ni Jaji wa Mahakama ya Rufaa.