Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Uhaba wa maji watishia mafanikio ya SDGs – Guterres

Uhaba wa maji watishia mafanikio ya SDGs – Guterres

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kwamba dunia ipo nyuma katika kutekeleza ahadi zake kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za kujisafi. Hivyo basi amezitaka serikali, sekta binafsi na jamii kuchukua hatua za haraka kukabiliana na uhaba unaoongezeka wa maji, uchafuzi wa mazingira na shinikizo linalotokana na mabadiliko ya tabianchi.

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu imo kwenye hotuba yake yenye kurasa saba aliyoitoa leo kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York, Marekani, mbele ya Mawaziri wanaoshiriki Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu kuhusu Malengo ya Maendeleo Endelevu, SDGs, wakati huu ambapo imesalia miaka minne kufikia ukomo wa malengo hayo mwaka 2030.

Hotuba yake ilijikita katika malengo matano yanayoangazia kwenye kikao hicho ambayo ni lengo namba 6 kuhusu maji safi na huduma za kujisafi, lengo namba 7 kuhusu nishati safi, namba 9 kuhusu viwanda, ubunifu na miundombinu, namba 11 kuhusu miji endelevu na namba 17 kuhusu ubia.

Mimi najikita zaidi na lengo kuhusu maji safi, salama na huduma za kujisafi ambalo alipatia kipaumbele zaidi akisema,  “mamia ya mamilioni ya watu wengi zaidi sasa wanapata huduma za maji ya kunywa na huduma usafi wa mazingira zinazodhibitiwa kwa usalama ikilinganishwa na miaka kumi iliyopita.

Hata hivyo, amesema kuwa dunia bado iko mbali kufikia lengo hilo linalotaka kila mkazi wa dunia awe na huduma hiyo ifikapo mwaka 2030 kwani, “takriban watu bilioni 2.2 bado hawana huduma za maji salama ya kunywa zinazosimamiwa kwa viwango vinavyofaa, na watu bilioni 3.5 hawana huduma za usafi wa mazingira zinazosimamiwa kwa usalama. Wakati huohuo, tunatumia rasilimali za maji kwa kiwango kinachozidi uwezo wa mzunguko wa asili wa maji kuzijaza upya.”

Ili kupunguza pengo linaloongezeka katika upatikanaji na usimamizi wa maji, Guterres amesema “serikali, sekta binafsi, wafanyabiashara na jamii lazima washirikiane kuziba mapengo yaliyopo katika ufadhili, ubunifu, miundombinu, uwezo wa kitaasisi na usimamizi wa huduma za maji, na kukabiliana na ongezeko la hatari zinazotokana na matumizi yasiyo endelevu ya maji na mabadiliko ya tabianchi.”

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, ameonya kwamba dunia ipo nyuma katika kutekeleza ahadi zake kuhusu upatikanaji wa maji safi na salama na huduma za kujisafi. Hivyo basi amezitaka serikali, sekta binafsi na jamii kuchukua hatua za haraka kukabiliana na uhaba unaoongezeka wa maji, uchafuzi wa mazingira na shinikizo linalotokana na mabadiliko ya tabianchi. Assumpta Massoi na maelezo zaidi.

Audio Credit
Assumpta Massoi
Sauti
3'29"
Photo Credit
© WHO