Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

21 APRILI 2026

21 APRILI 2026

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina Flora Nducha wa Idhaa hii anazungumza na mmoja wa walioshiriki mkutano wa CSW70, Masidis Scholastica Madowo Mbunge katika Bunge la Kaunti ya Siaya akiwakilisha kata ya South East Alego jimbo la Magharibi mwa Kenya, ili kuangazia kile anachokifanya kwenye Kaunti yake kuhakikisha wanawake wanapata haki hizo.

  1. Hii leo katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kutafanyika mdahalo wa wagombea wa nafasi ya Katibu Mkuu wa Umoja huo ambapo wagombea wanne wamejitokeza kuwania wawili wanaume na wawili wanawake. Wagombea hao ni Michelle Bachelet kutoka nchini Chile, Rafael Grossi kutoka nchini Argentina, Rebeca Grynspan kutoka Costa Rica, na Macky Sall kutoka nchini Senegal.
  2. Wakati huo huo Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Annalena Baerbock, amesema mchakato wa kumchagua Katibu Mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa ni hatua muhimu itakayoamua mwelekeo wa taasisi hiyo na mustakabali wa ushirikiano wa kimataifa. Akizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani kabla ya kuanza kwa mdahalo huo wa wazi, Baerbock ameeleza kuwa uchaguzi huo una umuhimu mkubwa duniani kote, ukigusa maisha ya zaidi ya watu bilioni nane, “Uamuzi huu si wa kiutawala tu, bali ni ujumbe kuhusu maadili na mwelekeo wa Umoja wa Mataifa katika kukabiliana na changamoto za dunia ya leo.”
  3. Takribani wahamiaji 8,000 waliripotiwa kufariki dunia au kutoweka duniani kote mwaka 2025, na kufanya jumla ya wahamiaji waliopoteza maisha tangu 2014 kufikia zaidi ya watu 82,000, hii imebainishwa katika takwimu mpya zilizotolewa leo na Shirika la Umoja wa Mataifa la Uhamiaji IOM. Takwimu hizo pia zinaonesha athari kubwa kwa familia, ambapo takribani watu 340,000 wameathirika moja kwa moja. IOM imeonya kuwa njia za uhamiaji si salama na zinazidi kuwa hatari.
  4. Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Mtaalam wetu Dkt. Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana na matumizi ya neno "UNYUMBA" 

Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!

Audio Credit
Rashid Malekela
Sauti
11'32"