Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

09 APRILI 2026

09 APRILI 2026

Pakua

Jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Kenya kusikia ujumbe wa Hanna Wendot Cheptumo Waziri wa Jinsia, Utamaduni na Maslahi ya Watoto wa Jamhuri ya Kenya ambaye alikuwa miongoni mwa washiriki wa CSW70 akieleza ni kwa namna gani Kenya inapiga hatua katika Lengo namba 5 la Usawa wa Kijinsia.

  1. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amelaani vikali mashambulizi makubwa ya anga yaliyofanywa na Israel dhidi ya Lebanon tarehe 8 Aprili, mashambulizi ambayo yamesababisha mamia ya raia kuuawa na kujeruhiwa, wakiwemo watoto, sambamba na kuharibu kwa kiasi kikubwa miundombinu ya kiraia. Taarifa iliyotolewa New York, Marekani na Msemaji wa Umoja wa Mataifa inamnukuu Guterres akionesha wasiwasi mkubwa kuhusu ongezeko la vifo miongoni mwa raia na kutoa pole kwa watu na Serikali ya Lebanon, akiwatakia nafuu ya haraka wale waliojeruhiwa.
  2. Katika tukio jingine hii leo, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amezindua Mfuko wa Urejeshaji wa Palestina uliopewa jina la Horizon Fund, akisisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua za haraka kusaidia wananchi wa Palestina kurejesha maisha yao na kujenga mustakabali bora. Akizungumza kupitia ujumbe wa video wakati wa uzinduzi uliofanyika Ramallah, huko Ukingo wa Magharibi eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel, Guterres amesema mfuko huo ni sehemu muhimu ya ushirikiano kati ya Umoja wa Mataifa na Taifa la Palestina.
  3. Wakati mgogoro wa Sudan ukikaribia kutimiza miaka mitatu, zaidi ya wakimbizi milioni moja wa Sudan walioko nchini Chad wanakabiliwa na hatari kubwa ya kupunguzwa kwa msaada muhimu wa kibinadamu. Onyo hilo limetolewa leo na mashirika mawili ya Umoja wa Mataifa ambayo ni lile la kuhudumia wakimbizi (UNHCR) pamoja na la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) wakitanabaisha kuwa huduma za msingi kama chakula, maji, malazi, ulinzi na huduma za afya zitalazimika kupunguzwa zaidi katika miezi ijayo iwapo pengo la ufadhili la dola milioni 428 halitazibwa haraka.

Mwenyeji wako ni Rashid Malekela, karibu!

Audio Credit
Rashid Malekela
Sauti
9'58"