Vijana lazima tubadili fikra ili kuleta mabadiliko chanya asema Mary Teye kutoka Ghana - CSW70
Sauti za vijana zinaendelea kusikika kwa nguvu katika wiki ya pili ya kikao cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani kinachofanyika hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo wanaharakati, watunga sera na wadau kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekusanyika kujadili namna ya kuendeleza haki , haki za kisheria na fursa kwa wanawake na wasichana.
Katika kikao cha mwaka huu cha CSW70, vijana hawapo tu kama washiriki bali pia wanahamasisha mabadiliko.
Washiriki kutoka kila pembe ya duniani wanabadilishana mawazo, kujenga mitandao na kusisitiza hatua madhubuti za kuimarisha haki za wanawake, ulinzi wa kisheria na hatua za kuhakikisha haki zao hazikiukwi.
Miongoni mwao ni Mary Teye, mjasiriamali kijana kutoka Ghana na mkurugenzi wa kampuni ya ubunifu wa mavazi na mitindo ya AWULAK. Anasema mkutano huo wa kimataifa unatoa fursa muhimu kwa wanawake hasa vijana kuunganishwa na kupaza sauti zao.
“Jukwaa hili limewapa nafasi wanawake vijana kama mimi na nilikotoka kuungana na wanawake wanaofanya mabadiliko katika sehemu mbalimbali za dunia.”
Mary anasema mkutano huo pia unaimarisha harakati za vijana wanaotaka kuona haki za wanawake zikitekelezwa kwa vitendo katika jamii zao.
Anaamini maendeleo hayatategemea tu sera na sheria mpya, bali pia mabadiliko ya mitazamo na kuwawezesha wanawake vijana kuamini uwezo wao.
“Kila kitu unachofanya kinaanzia akilini mwako. Tumezungumza sana na kutekeleza sera nyingi, lakini mambo hayatabadilika hadi tubadilishe namna tunavyofikiri na mitazamo yetu kuhusu utekelezaji wa sera hizo.”
Mary amewahimiza vijana wenzie kuwa cha muhimu ni kujiamini na kutambua kuwa wana uwezo wa kuleta mabadiliko chanya katika jamii zao.
“Kitu kingine ninachoweza kusema ni kwamba lazima ujiamini. Unaweza kusikia mambo mengi watu wakisema, lakini kama hujielewi na kujiamini, hutaweza kuleta mabadiliko yoyote.”
Mary pia amesisitiza umuhimu wa haki kupatikana kwa wakati kwa waathirika wa ukatili na ubaguzi.
Ameonya kuwa haki inapocheleweshwa inaweza kuwakatisha tamaa waathirika kujitokeza na kutafuta msaada.
Wakati viongozi wa dunia wakiendelea kujadili sera na ahadi katika CSW70, washiriki vijana kama Mary wanasema mabadiliko ya kweli yatatokea pale ahadi zitakapotekelezwa kwa vitendo na majukwaa zaidi yatakapoundwa ili wanawake na wasichana waweze kuongoza mabadiliko.
Kikao hicho cha wiki mbili kinaendelea hadi tarhe 19 Machi.
Sauti za vijana zinaendelea kusikika kwa nguvu katika wiki ya pili ya kikao cha 70 cha Kamisheni ya Hali ya Wanawake duniani kinachofanyika hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa jijini New York Marekani ambapo wanaharakati, watunga sera na wadau kutoka sehemu mbalimbali za dunia wamekusanyika kujadili namna ya kuendeleza haki , haki za kisheria na fursa kwa wanawake na wasichana. Flora Nducha amepata fursa ya kuzungumza na mmoja wa vijana washiriki kutoka Ghana na kutuandalia taarifa hii