Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Vijana wachagiza hatua za haraka kuhusu haki za wanawake katika mkutano wa CSW70

Vijana wachagiza hatua za haraka kuhusu haki za wanawake katika mkutano wa CSW70

Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake Duniani CSW70 leo unaendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York ukiwa umeingia siku ya 3. Na vijana hawakusahaulika wamepewa nafasi ya kutoa maoni yao na mapendekezo yao kuhusu maudhui ya mwaka huu ambayo yanasisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuhusu haki za wanawake, usawa wa kisheria na ushiriki wa vijana. 

Katika mkutano huu wa kila mwaka Kwa wajumbe wengi vijana, si wa majadiliano pekee bali ni nafasi ya kuhakikisha wanawake hasa vijana wanashiriki kikamilifu katika kutafuta suluhu za changamoto za dunia.

Eunice Kisua Ajan, mwanaharakati kijana mwenye asili ya Ghana na anayeishi hapa Marekani, anasema vijana wanawake hawapaswi kuwa washiriki wa alama tu, bali wanahitaji kuwa sehemu ya uongozi katika masuala muhimu kama katika kila nyanja.

"Hatuko hapa kuwa kama ishara ya mfano tu. Tuko hapa kuzungumzia ushiriki wa wanawake katika amani na usalama, ushiriki wa wanawake katika hatua za tabianchi… kwa sababu bila sisi kizazi kijacho hakiwezi kuendelea kuwepo. Ndoto zenu ni muhimu, maisha yenu ni muhimu na thamani yenu ni kubwa kuliko tu sunza nzuri”."

Ajan anasema kuwa kuwapa nguvu vijana wanawake kuzungumza na kushika nafasi za uongozi ni muhimu katika kujenga jamii jumuishi zenye haki na, haki ya kisheria na hatua zaidi.

Mshiriki mwingine kijana, ni Taslimat Yusuf kutoka Nigeria, anahudhuria mkutano huo ili kuangazia changamoto zinazoendelea katika jamii yake kama ukeketaji wa wasichana na ukatili wa kijinsia. Anawakilisha shirika la Shirika la Sauti Moja kwa Ukombozi wa Wanawake na Watoto au One Voice Initiative for Women and Children Emancipation.

Tissouf anasema manusura wa ukatili katika jamii yake mara nyingi huogopa kuzungumza kutokana na hofu na unyanyapaa, hivyo amesisitiza katika jukwaa hili kwamba kuna haja kubwa ya mifumo madhubuti ya msaada.

"Tunahitaji kuwapa manusura sauti na kuwajulisha kuwa hawako peke yao, wanaonekana na sauti zao zitasikika. Haki lazima itendeke kwao na hii ndio sababu niko hapa kuchagiza uelewa kuhusu ukeketaji, ukatili wa kijinsia na kuona jinsi ambavyo nitaweza kubadilishana mawazona washiriki wengine."

Taslimat pia anazitaka serikali kushirikiana na mashirika ambayo tayari yanafanya kazi ya kusaidia manusura wa vitendo hivyo badala ya kuanzisha taasisi mpya zinazoweza kurudia kazi zilizopo. Anasema kupanua wigo vituo vya msaada kwa waathirika wa ukatili wa kijinsia kutasaidia waathirika kupata msaada na haki kwa haraka.

Kadri mkutano huo unavyoendelea, wanaharakati vijana wanasema ujumbe wao kwa viongozi ni wazi: ahadi lazima zibadilishwe kuwa hatua halisi ili kuleta maendeleo ya kweli kwa wanawake na wasichana duniani.

Pakua

Mkutano wa 70 wa Kamisheni ya Hali ya wanawake Duniani CSW70 leo unaendelea hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa New York ukiwa umeingia siku ya 3. Na vijana hawakusahaulika wamepewa nafasi ya kutoa maoni yao na mapendekezo yao kuhusu maudhui ya mwaka huu ambayo yanasisitiza umuhimu wa kuchukuliwa kwa hatua madhubuti kuhusu haki za wanawake, usawa wa kisheria na ushiriki wa vijana. Flora Nducha amekutana na baadhi yao kusikia maoni yao

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
3'26"
Photo Credit
UN News