23 OKTOBA 2025
Pakua
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoangazia siku ya Umoja wa Mataifa na tutasikia kutoka mashinani wananchi na asasi za kiraia zina yapi ya kusema kuhusu shirika hili kubwa na la kipekee linalounganisha nchi wanachama 193 duniani.
- Mashirika manne ya Umoja wa Mataifa lile la uhamiaji IOM, la kuhudumia wakimbizi UNHCR, la Kuhudumia watoto UNICEF na la mpango wa chakula duniani WFP leo yametoa wito wa dharura kwa dunia kuchukua hatua mara moja kukabiliana na janga la kibinadamu linaloongezeka nchini Sudan. Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada, nchini humo wakiwemo watoto milioni 15 na wakimbizi karibu milioni moja.
- Mahakama ya Kimataifa ya Haki (ICJ) jana Oktoba 22 ilisema Israeli lazima itimize majukumu yake kama “anayekalia kimabavu” kwa kuhakikisha kuwa msaada unaweza kupita bila vizuizi na kwa kuheshimu haki za Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya kibinadamu yanayofanya kazi katika Ardhi ya Palestina Iliyokaliwa kwa Mabavu. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameelezea maoni hayo ya ICJ kuwa “muhimu sana,” akiongeza kuwa yametolewa wakati ambapo Umoja wa Mataifa unafanya kila juhudi kuongeza kasi ya misaada kuingia Gaza baada ya kusitishwa kwa mapigano.
- Nchini Kenya, wahudumu wa afya waliokuwa wakisubiri hadi siku 15 kupata malipo sasa wanapokea pesa ndani ya saa 72 pekee, shukrani kwa mfumo mpya wa malipo ya kidijitali uliotolewa na Shirika la Sfya la Umoja wa Mataifa WHO na Wizara ya Afya ya nchi hiyo. Mfumo huu unapeleka fedha moja kwa moja kwenye pochi za simu za wafanyakazi, ukipunguza ucheleweshaji, gharama na kuongeza motisha. Wafanyakazi zaidi ya 120,000 sasa wanafaidika, kuboresha ufanisi wa kampeni za chanjo na juhudi za kudhibiti polio.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
15'53"