Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mateka waachiliwa Gaza, misaada yaanza kuingia - UN

Mateka waachiliwa Gaza, misaada yaanza kuingia - UN

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, leo amekaribisha kwa furaha kuachiliwa kwa mateka wote waliokuwa hai kutoka Gaza, huku mashirika ya misaada yakiripoti kwamba usambazaji wa misaada ya kuokoa maisha sasa unafanyika na misaada inaingia kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya na vita.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema amepokea kwa “faraja kubwa” kuachiliwa kwa mateka hao, miaka miwili tangu walipotekwa wakati wa mashambulio ya Hamas nchini Israel.
Amesema hatua hiyo ni mwanzo wa matumaini mapya, lakini bado kuna kazi kubwa mbele ya kurejesha utu na usalama Gaza.

Kali hiyo imeungwa mkono na Afisa wa Shirika la Umoja wa mataifa la Kuratibu Misaada ya Kibinadamu Olga Cherevko akizungumza na UN News amesema “Sasa wanaweza kuzungumzia mustakabali wa familia zao kwa mara ya kwanza kwa miezi, kwani muda wote walikuwa wakiishi kwenye hofu ya vita”

Hayo yanajiri wakati mashirika ya Umoja wa Mataifa yakiripoti ongezeko kubwa la usambazaji wa misaada.

Shirika la OCHA limesema limepata idhini ya kuingiza tani 190,000 za chakula, dawa, vifaa vya makazi na misaada mingine muhimu kiwango kikubwa zaidi tangu mapigano kuanza.

Kwa mara ya kwanza tangu Machi, gesi ya kupikia pia imeruhusiwa kuingia Gaza. Olga anasema “ Watu wote wako na matumaini makubwa kwa siku za usoni, hata kama changamoto za maisha bado zipo. Nilizungumza na familia moja iliyokuwa katika hema lililoharibiwa vibaya kando ya barabara, na walinialika kula chakula cha mchana na supu ya nyanya iliyochemshwa walisema hii ndio mara ya kwanza kupata chakula safi wakiweza kuipika wenyewe”

OCHA imesema kuruhusiwa kwa misaada  kumeboresha uwezo wa timu za misaada kufika katika maeneo yaliyokuwa magumu kufikika, na sasa zinaweza kusambaza huduma za afya, maji na makazi kwa maelfu ya familia zilizo hatarini.

Mpango wa Umoja wa Mataifa wa siku 60 za kwanza za usitishaji mapigano unalenga kufikisha misaada ya chakula, elimu, na huduma za afya kwa karibu kila mtu ndani ya Gaza.’Kwa mujibu wa Olga ni hatua inayoleta matumaini makubwa kwa watu wa Gaza “Hisia ni chanya sana, na sisi tunaendelea kufanya kazi, kusambaza misaada na kuongeza juhudi ili kufikia familia kama hii, kwani mahitaji bado ni makubwa sana, na kazi yetu inaanza tu. Lakini tuko tayari na tumejizatiti kuwa pamoja na watu kila hatua ya njia.”

Pakua

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, António Guterres, leo amekaribisha kwa furaha kuachiliwa kwa mateka wote waliokuwa hai kutoka Gaza, huku mashirika ya misaada yakiripoti kwamba usambazaji wa misaada ya kuokoa maisha sasa unafanyika na misaada inaingia kwa kiwango kikubwa katika eneo hilo lililoharibiwa vibaya na vita: Flora Nducha amefuatilia na hii hapa taarifa yake

Audio Credit
Flora Nducha
Sauti
2'56"
Photo Credit
© WHO