Wadau wa afya wazindua muongozo mpya wa kukomesha vifo vinavyotokana na kutokwa damu baada ya kujifungua
Mashirika ya afya duniani yametoa miongozo mipya yenye lengo la kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake wanaopoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua hali inayojulikana kama postpartum haemorrhage au PPH. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi.
Mwongozo huo umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO), Shirikisho la Wakunga Duniani (ICM) na Shirikisho la Kimataifa la Madaktari wa wanawake na Uzazi (FIGO)
Kila mwaka, takribani wanawake 45,000 hufariki duniani kutokana na tatizo hili. Vifo hivi vinaweza kuzuilika endapo huduma sahihi zitapatikana kwa wakati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mwongozo huo mjini Cape Town, Afrika Kusini, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus, amesema
“Leo tunasherehekea hatua muhimu katika historia ya afya ya uzazi. Katika kongamano hili, kwa kushirikiana na FIGO na ICM, WHO inajivunia kuzindua kwa pamoja mwongozo mpya wa WHO wa kukabili kutokwa damu baada ya kujifungua. Mwongozo huu unajumuisha mapendekezo 51 kuhusu chanzo hiki kikuu cha vifo vya akina mama, ukigusa maeneo ya kinga, utambuzi, matibabu na huduma saidizi. Pia umeleta ufafanuzi mpya wa kitaalamu wa PPH, ukitokana na uchambuzi mkubwa zaidi wa kimataifa wa takwimu zilizowahi kufanyika. Hii ni hatua kubwa mbele, utambuzi wa mapema, hatua za haraka, na maisha mengi zaidi kuokolewa.”
Miongozo mipya inapendekeza mabadiliko makubwa katika utambuzi wa PPH. Watoa huduma sasa wanashauriwa kuchukua hatua haraka pindi damu inapofikia mililita 300, au dalili zisizo za kawaida za mwili zinapoonekana badala ya kungoja hadi damu ifikie mililita 500 kama ilivyokuwa awali.
Vifaa rahisi vya kupima kiwango cha damu vinapendekezwa kutumika mara moja baada ya kujifungua.
Mara tu PPH inapothibitishwa, mwongozo unapendekeza utekelezaji wa hatua zinazojulikana kama MOTIVE bundle, ikiwemo:
- Kukandamiza mfuko wa uzazi,
- Kutoa dawa za kuongeza mikazo ya mfuko wa uzazi,
- Kutumia dawa ya kupunguza damu (tranexamic acid),
- Kutoa maji kupitia mishipa ya damu,
- Kuchunguza njia ya uke na sehemu ya uzazi, na
- Kusogeza mgonjwa kwenye huduma ya dharura endapo kutokwa damu kunaendelea.
Vilevile, miongozo hiyo inahimiza kuimarishwa kwa huduma za ujauzito na baada ya kujifungua, ikiwemo matibabu ya upungufu wa damu.
Mashirika ya afya duniani yametoa miongozo mipya yenye lengo la kuokoa maisha ya maelfu ya wanawake wanaopoteza maisha kutokana na kutokwa damu nyingi baada ya kujifungua hali inayojulikana kama postpartum haemorrhage au PPH. Tupate taarifa zaidi kutoka kwa Leah Mushi.