UNESCO: Uongozi shirikishi ni muhimu kwa mafanikio ya walimu na matokeo ya wanafunzi
Uongozi wa kugawana majukumu na mashauriano ya kina na walimu ni mambo muhimu katika kuboresha ustawi wa waelimishaji na matokeo ya kujifunza ya wanafunzi, amesema Carlos Vargas, Mkuu wa Kitengo na Mkuu wa Sekretarieti ya Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Walimu kwa Elimu 2030 katika UNESCO.
UNESCO ni shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni ambalo kupitia maadhimisho ya siku ya walimu duniani Oktoba 5, ilitangaza kaulimbiu kuwa ni Kubadilisha ualimu kuwa taaluma ya ushirikiano, ikisisitiza uwezo wa kubadilisha hali kupitia ushirikiano kwa walimu, shule na mifumo ya elimu.
Bwana Vargas kupitia mahojiano yaliyochapishwa kwenye chaneli ya YouTube ya UNESCO katika kuthibitisha umuhimu wa kushirikisha walimu akarejelea utafiti uliofanyika katika nchi 19 za Amerika Kusini na Karibea kuhusu matokeo ya kujifunza ambapo ilionekana kwamba..
"Shule zilizofanya vizuri zaidi zilikuwa zile ambazo uongozi wa shule ulikuwa shirikishi, ukishauriana na walimu ambao walikuwa wakishirikiana na jamii. Kwa hiyo mwisho wa siku, mtu anagundua kwamba uongozi mzuri wa shule una matokeo, si tu katika hali ya mazingira ya shule na ustawi wa walimu, bali pia katika matokeo bora ya kujifunza kwa wanafunzi. Hiyo ndiyo aina ya kazi ambayo viongozi wa shule wanaweza kufanya."
Na alipoulizwa iwapo Akili Mnemba au Unde itaondoa nafasi ya mwalimu, Bwana Vargas amesema:
“Kwa hivyo nadhani akili unde, kama tunavyoanza kuona, ina uwezo wa kupunguza mzigo wa kazi wa walimu ili waweze kujitolea kikamilifu kwenye kipimo hiki cha uhusiano na hisia katika kufundisha wanafunzi, ambacho tunajua ni muhimu sana. Lakini jinsi ya kushirikisha wanafunzi, kuwasaidia kufikiria kazi watakayopenda kufanya baadaye, kufundisha kulingana na mahitaji ya mwanafunzi, ningesema, ni jukumu ambalo walimu watabakia nalo."
Uongozi wa kugawana majukumu na mashauriano ya kina na walimu ni mambo muhimu katika kuboresha ustawi wa waelimishaji na matokeo ya kujifunza ya wanafunzi, amesema Carlos Vargas, Mkuu wa Kitengo na Mkuu wa Sekretarieti ya Kikosi Kazi cha Kimataifa cha Walimu kwa Elimu 2030 katika UNESCO.