30 SEPTEMBA 2025
Pakua
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayomulika ujumbe wa Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki EAC, Veronica Nduva ambaye alizungumza na Flora Nducha kandoni mwa UNGA80. Pia tunakuletea muhtasari wa habari kama zifuatazo.
- Ikiwa ni zaidi ya miaka minane tangu zaidi ya wakimbizi 750,000 waislamu wa kabila la warohingya wakimbie Myanmar kuelekea kwenye kambi kubwa nchini Bangladesh, mgogoro huo bado haujapatiwa suluhisho na leo hapa makao makuu ya Umoja wa Mataifa viongozi wamekutana kusaka suluhu ya kudumu kwa warohingya na makabila mengine madogo nchini Myanmar. Katibu Mkuu Antonio Guterres kupitia Afisa Mtawala Mkuu wa UN Courtenay Rattray amesema, “mgogoro huu, ambao umezidi kuongezeka tangu mapinduzi ya kijeshi Myanmar ya mwaka 2021, unasigina haki za binadamu, utu na usalama wa mamilioni ya watu na unatishia uthabiti wa kikanda. Haitoshi tu kutathmini hali ilivyo. Tunapaswa pia kuendeleza mshikamano na kubuni suluhisho.”
- Amani nchini DRC imesalia bado ahadi, ni kauli ya Bintou Keita, Mwakilishi Maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC aliyotoa wakati akihutubia Baraza la Usalama lililokutana leo kujadili hali Mashariki mwa DRC. Anasema hali inazidi kuwa tete. “Ghasia zinaendelea kushamiri jimboni Kivu Kaskazini hususan eneo la Rutshuru tangu waasi wa M23 watwae eneo hilo. Kuanzia mwezi Juni na kuendelea ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani, MONUSCO umepokea maombi lukuki ya watu wakitaka ulinzi kwenye maeneo yanayodhibitiwa na M23.”.
- Na mashirika ya Umoja wa Mataifa leo yamesisitiza wito wa kupatikana kwa sitisho la mapigano huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa kimabavu na Israel, ili kupunguza machungu wakati huu ambapo Mpango wa Marekani wa Vipengele 20 unaibua matumaini ya kukomeshwa kwa mapigano. Ricardo Pires, msemaji wa shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia watoto, UNICEF amesema, “ni muhimu tupate sitisho la mapigano na misaada iweze sio tu kuingia na kuepusha baa la njaa, bali pia kuelekezwa maeneo ya kusini. Lakini vile vile kuhakikisha watoto na familia zao wanapata malazi bora wakati huu majira ya baridi kali yanakaribia. La sivyo italeta zahma ya afya kwa watoto na familia zao.”.
Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!
Audio Credit
Leah Mushi
Audio Duration
12'3"