ECSA: Diplomasia ya kisayansi kutumika kusongesha Mkataba wa Zama Zijazo Afrika
Katika siku ya pili ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, kando ya hotuba, viongozi wa nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA-HC watakuwa na mkutano wa kusongesha diplomasia ya kisayansi ili kuhakikisha bara la Afrika haliachwi nyuma kwenye kukabiliana na changamoto za kiafya, baada ya kujifunza kutokana na coronavirus">COVID-19 au UVIKO19.
Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Dkt. Ntuli Kapologwe akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa hii ametaja wanachotarajia kwenye mkutano huo kuwa ni maazimio mawili. Azimio la kwanza ni kujenga kituo cha ufanisi na kituo mahiri cha masuala ya kuendeleza sayansi kwa upande wa Afrika ambacho kitajengwa mkoani Arusha, kaskazini mwa Tanzania ambako ndiko makao makuu ya ECSA -HC.
“Azimio la pili ni kuongeza uwekezaji wa rasilimali fedha kwenye masuala ya sayansi na utafiti kwa upande wa Afrika, ili sasa tuweze kushindana kuwa ni bara lenye ushindani na mabara mengine kwenye eneo la sayansi. Na hiyo ndio diplomasia ya sayansi,” amesema Dkt. Kapologwe.
Kuhusu kutumia diplomasia ya kisayansi kusongesha Mkataba wa Zama Zijazo, Dkt. Kapologwe amesema “kwa sasa ni muhimu na ndio suala la mpito tukitoka katika Maendeleo Endelevu ambayo tunatekeleza kwa miaka 15. Kwa maana mwaka 20230 tutaenda kwenye Mkataba za Zama Zijazo ambazo hizo zama zitahitaji sana sayansi.”
Amesema ni kwa kutambua hilo ndio maana ECSA-HC tunaona huu ndio muda muafaka kabla ya kufikia mwaka 2030 tuwe tayari tumeweza kufanya na kuanzisha mijadala ya aina hii ambayo itasaidia kuleta chachu kwa nchi zote za Afrika ili kuwekeza katika sayansi na diplomasia.
Idhaa ya Umoja wa Mataifa ilitaka kufahamu kipi kinachoweza kusongesha haraka ndoto ya ECSA kwani muda mrefu wameshindwa kutekeleza hilo? Dkt. Kapologwe ametaja utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa jumuiya.
“Fursa iliyopo ni tayari kuna ari nzuri ya kisiasa na pia kuna viongozi ambao wanapenda sayansi. Na pili, Tanzania imetoa eneo eneo ambapo yatajengwa vituo mbali mbali vya umahiri vinavyoweza kusaidia masuala na wataalamu kutoka katika maeneo mbalimbali. Yote haya yanatufanya tuwe na imani kubwa kwamba tutakuwa na kituo na pia tuweze kusukuma diplomasia ya kisayansi, sio tu kwa upande wa Bara Afrika na ulimwenguni kote,”ametamatisha Mkurugenzi Mkuu huyo wa ECSA-HC.
Mkutano umeandaliwa na ECSA kwa kushirikiana na serikali ya Tanzania ambapo Dkt. Phillip Mtango , Makamu wa Rais wa Taifa hilo la Afrika Mashariki anayemwakilisha Rais wa Tanzania, Samia Sulhu Hassan kwenye UNGA80 anatarajiwa kushiriki.
ECSA-HC iliyoundwa mwaka 1974 kusongesha ushirikiano wa kikanda unajumuisha nchi 9 ambazo ni Kenya, Lesotho, Malawi, Mauritius, Eswatini, Tanzania, Uganda, Zambia na Zimbabwe.
Katika siku ya pili ya Mjadala Mkuu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, UNGA, kando ya hotuba, viongozi wa nchi 9 wanachama wa Jumuiya ya Afya ya Mashariki, Kati na Kusini mwa Afrika, ECSA watakuwa na mkutano wa kusongesha diplomasia ya kisayansi ili kuhakikisha bara la Afrika haliachwi nyuma kwenye kukabiliana na changamoto za kiafya, baada ya kujifunza kutokana na COVID-19 au UVIKO19. Mkurugenzi Mkuu wa ECSA Dkt. Ntuli Kapologwe akihojiwa na Assumpta Massoi wa Idhaa hii ametaja wanachotarajia kwenye mkutano huo..