22 SEPTEMBA 2025
Pakua
Hii leo jaridani tunaangazia ujumbe wa washirirki ya mkutano wa 80 wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, hasa maadhimisho ya miaka 80 ya umoja huo. Pia tunamulika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi.
- Umoja wa Mataifa hii leo umeadhimisha miaka 80 tangu kusainiwa kwa Mkataba wake tarehe 26 Juni 1945, tukio lililotoa matumaini mapya kwa dunia iliyokuwa imechoka kutokana na vita viwili vya dunia, mauaji ya halaiki na ukoloni. Katika maadhimisho hayo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amesema kumbukizi ya kuanzishwa kwa UN ni fursa ya kukumbuka ujasiri wa waanzilishi wa taasisi hiyo na kuimarisha mshikamano wa kimataifa katika kukabili changamoto zinazokabili dunia hivi sasa.
- Tukisalia na maadhimisho ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa , moja ya mchango mkubwa unaotoa kwa dunia tangu ulipoanzishwa mwaka 1945 ni kusaidia mamilioni ya watu wanaolazimika kufungasha virago kukimbia makwao na kuwa wakimbizi kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo vita. Uganda ni moja ya nchi zinazohifadhi maelfu ya wakimbizi wengi kutoka Sudan, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC wakisaidiwa chini ya shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi UNHCR na mengine. John Kibego kutoka Radio washirika Kazi-Njema FM iliyoko mjini Hoima Uganda amepata fursa ya kuzungumza na mmoja wa wakimbizi hao akielezea mchango mkubwa wa Umoja wa Mataifa kwake.
- Kando ya maadhimisho ya siku ya miaka 80 ya Umoja wa Mataifa, hapa makao makuu kumefanyika mashauriano ya faragha yenye lengo la kusaka majawabu ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi. Mashauriano ya leo ni sehemu ya mashauriano 10 yatakayofanyika kuelekea mkutano wa tabianchi wa wakuu wa nchi na serikali utakaofanyika keshokutwa Jumatano hapa Umoja wa Mataifa. Assumpta Massoi amezungumza na mmoja wa watoa mada kwenye mashauriano hayo ambayo matokeo yake yatawasilishwa kwenye mkutano wa viongozi.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Audio Credit
Anold Kayanda
Sauti
11'24"