UNICEF yahimiza Taliban kuruhusu wasichana Afghanistan kuendelea na masomo
Tarehe kama ya leo, 18 Septemba mwaka 2021 dunia ilishitushwa na kuhuzunishwa na tangazo lililotolewa la uongozi wa Taliban nchini Afghanistan la kukataza wasichana barubaru kuendelea na masomo na kwamba darasa la sita ndio mwisho wa elimu yao. Sasa ni miaka minne na katazo hilo bado limesimama kitu ambacho Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa ni “moja ya dhulma kubwa za wakati wetu.”
Majira haya, mwezi Septemba ni muda wa shule nyingi kufunguliwa duniani kote, watoto wakiwa na furaha na shauku ya Kwenda shule kujifunza lakini hali ni tofauti kwa wasichana wa Afghanistan ambao licha ya juhudi kubwa za kushawishi uongozi wa Taliban kuruhusu waweze kuendelea na masomo baada ya kuhitimu darasa la sita, bado wamegonga mwamba.
Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF, Catherine Russell, katika taarifa yake aliyoitoa hii leo jijini New York Marekani ametahadharisha vikali kuhusu marufuku inayoendelea ambayo imewazuia kwa kipindi cha miaka minne sasa wasichana balehe nchini Afghanistan kuhudhuria shule akiiita “tishio kubwa” kwa mustakabali wa taifa hilo.
Kwa mujibu wa UNICEF, kufikia mwisho wa mwaka huu 2025, zaidi ya wasichana milioni 2.2 wa Afghanistan watakuwa wamenyimwa haki ya kupata elimu zaidi ya darasa la sita. Idadi hiyo inatarajiwa kuongezeka zaidi kufuatia kurejea kwa zaidi ya Waafghanistani milioni mbili kutoka nchi jirani mwaka huu, hali inayoongeza changamoto za upatikanaji wa elimu.
Kupitia ujumbe wake uliochapishwa leo na UNICEF jijini New York, Marekani,
Mkuu huyo wa UNICEF amesema wakati mamilioni ya watoto kote ulimwenguni wanarejea shuleni mwezi huu, wasichana wa Afghanistan wanaendelea kunyimwa haki ya msingi ya elimu, hali ambayo anaitaja kama “moja ya dhulma kubwa za wakati wetu.” Ameonya kuwa kuzuia elimu kwa nusu ya idadi ya watu kunadhoofisha uthabiti wa muda mrefu na maendeleo ya kiuchumi ya taifa.
Kiongozi huyo wa UNICEF pia ameeleza wasiwasi kuhusu athari za kijamii za marufuku hiyo, akitaja ongezeko la changamoto za afya ya akili, ndoa za utotoni na viwango vya juu vya uzazi miongoni mwa wasichana waliolazimishwa kubaki majumbani.
Amesema “Wasichana wa Afghanistan wanapoteza zaidi ya masomo darasani; wananyimwa mawasiliano ya kijamii, ukuaji binafsi, nafasi ya kuunda mustakabali wao na kutimiza uwezo wao.”
UNICEF inatoa wito wa haraka kwa mamlaka za Afghanistan kuondoa marufuku hii na kuruhusu kila msichana nchini Afghanistan kupata elimu kuanzia shule ya msingi hadi sekondari na kuendelea.
Tarehe kama ya leo, 18 Septemba mwaka 2021 dunia ilishitushwa na kuhuzunishwa na tangazo lililotolewa la uongozi wa Taliban nchini Afghanistan la kukataza wasichana barubaru kuendelea na masomo na kwamba darasa la sita ndio mwisho wa elimu yao. Sasa ni miaka minne na katazo hilo bado limesimama kitu ambacho Umoja wa Mataifa umeeleza kuwa ni “moja ya dhulma kubwa za wakati wetu.” Leah Mushi na taarifa zaidi.