Agizo jipya la kuhamisha watu katika ukanda wa Gaza ni ‘msumari wa moto kwenye kidonda’
Wakati Israeli ikiwa imetoa amri mpya ya watu kuhama kutoka jiji la Gaza katika eneo inalokalia kimabavu la Palestina, na kuelekea eneo ililotenga na kuliita ukanda wa kibinadamu kusini mwa Ukanda wa Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO limesikitishwa na agizo hilo jipya ikisema eneo halina ukubwa wala huduma za kutosha kusaidia wale walioko tayari huko, sembuse wale watakaowasili. Huduma za afya ni tete.
Ndani ya shoroba za hospital ya Al Shifa iliyoko jiji la Gaza, na tarehe ni 14 mwezi huu wa Septemba, wagonjwa mahututi wamebebwa mzobemzobe, wakiwa na maumivu makali.
Mlundikano ni mkubwa,ndani ya wodi hapa na damu imetapaa sakafuni.
Kando ni mgonjwa amewekewa mashine ya kumsaidia kupumua, naye yuko hoi bin taaban.. mwingine ana kiwewe.. anatikisa miguu yake …
Daktari anachutama na kuanza kufuta damu kwa mmoja wa wagonjwa aliyelala sakafuni, angalau kupunguza mmiminiko wa damu.
Kamera inasogea karibu, hapa mama mmoja amejifunika ushungi lakini umetapakaa damu… mbele yake binti mdogo naye uso mzima umetapakaa damu.
Pembeni kwenye sakafu majeruhi mmoja akaeleza masahibu yaliyomfika
“Wakati naelekea nyumbani, nilipigwa risasi mguuni. Hali hapa hospitali ni ngumu mno. Hakuna madaktari, hakuna vitanda. Nimelala hapa chini kwa zaidi ya saa moja sasa na siwezi kufanya chochote. Nimechoka na risasi iko mguuni. Sijui la kufanya! Nimechoka mno hakika. Enyi binadamu tusaidieni, tuokoeni, tutazameni. Hali hapa hospitali Gaza ni mbaya.”
Dkt. Ismail Ramadan, anahudumia kitengo cha wagonjwa mahututi kwenye hospitali hii ya Al Shifa na anakiri kuwa hali ni mbaya akisema, “bila shaka. Kutokana na maagizo ya mara kwa mara ya kuhama kutoka Ukanda wa Gaza, na hosptali nyingi hazitoi huduma, kama vile hospitali ya Baptist, idadi ya majeruhi na wagonjwa wanaofika hapa Al Shifa inaongezeka. Na kama unavyoona mwenyewe, idadi ya watu ni kubwa na watu wamelundikana kwenye vitanda. Hakuna vitanda vya kutosha kwa wagonjwa na hivyo tunalazimika kuhudumia wagonjwa wakiwa sakafuni. Vyumba vya upasuaji navyo havitoshi. Kwa sasa tuna vyumba vitatu tu. Tuna idadi kubwa ya majeruhi. Kwa Bahati mbaya, tunabidi kuchagua ni nani ahudumiwe na nani asihudumiwe. Ni kati ya kuokoa maisha kati ya watoto na wazee.”
Kutoka Al Shifa nakupeleka moja kwa moja hadi hospital ya watoto ya Al Rantisi hapa hapa jiji la Gaza. Watoto wako taabani kwenye mashine za kuwasaidia kupumua. Miongoni mwao mtoto Moutasem Arafa anayepambania uhai wake. Saeed Nahed Saeed anajitambulisha …
“Mimi ni baba wa Moutasem Arafa, mtoto mwenye umri wa mwaka mmoja na miezi minane ambaye ana tatizo kubwa la figo zote mbili kushindwa kufanya kazi. Sasa yuko hapa kwenye wodi ya wagonjwa mahututi. Hali kwenye hospitali katika mazingira haya tunamoishi ni ngumu. Hali ya mtoto wangu inakuwa mbaya kila uchao, na ninahofia kuwa ninaweza kumpoteza.”
WHO inatoa wito kwa ulinzi wa vituo vya afya, wahudumu wa afya na raia huku ikisema janga linalochochewa na binadamu wajibu ni wa kila mtu kulidhibiti, kauli inayokuja wakati Kamisheni ya Umoja wa Mataifa imetangaza kuwa Israeli imetekeleza mauaji ya halaiki huko Gaza.
Wakati Israeli ikiwa imetoa amri mpya ya watu kuhama kutoka jiji la Gaza katika eneo inalokalia kimabavu la Palestina, na kuelekea eneo ililotenga na kuliita ukanda wa kibinadamu kusini mwa Ukanda wa Gaza, shirika la Umoja wa Mataifa la Afya duniani, WHO limesikitishwa na agizo hilo jipya ikisema eneo halina ukubwa wala huduma za kutosha kusaidia wale walioko tayari huko, sembuse wale watakaowasili. Huduma za afya ni tete kama anavyosimulia Flora Nducha kwa taarifa hii.