28 AGOSTI 2025
Pakua
Jaridani leo tunakuletea mada kwa kina, wiki ya Maji ikifikia tamati leo Agosti 28 na maudhui yakiwa Maji kwa ajili ya Hatua kwa Tabianchi, tunabisha hodi kaunti ya Kajiado nchini Kenya kumsikia mtendaji kwenye mradi wa maji wa Kerarapon Water Association ambalo ni shirika la kijamii linalohusika na maji na mazingira huko kaunti ya Kajiado nchini Kenya. Mengine ni kama yafuatayo.
- Ukraine ambapo leo Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres ameungama na mashirika mengine ya Umoja wa Mataifa kulaani vikali mashambulizi ya makombora na ndege zisizo na rubani droni yaliyofanywa na Urusi usiku kucha kuamkila dhidi ya miji ya Ukraine na kusababisha vifo na majeruhi kwa raia, wakiwemo watoto, na pia kuharibu majengo ya kidiplomasia jijini Kyiv. Amesisitiza kuwa mashambulizi dhidi ya raia na miundombinu yao yanakiuka sheria za kimataifa za kibinadamu, akitaka yakome mara moja na kurudia wito wake wa kusitisha mapigano ili kuelekea amani ya kudumu itakayoheshimu uhuru wa watu, uhuru wa kitaifa na mipaka ya Ukraine kama inavyotambuliwa kimataifa.
- Kuhusu Mashariki ya Kati Katibu Mkuu António Guterres akizungumza na waandishi wa Habari hii leo kwenye Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa ameonya kuwa operesheni za kijeshi mjini Gaza zitakuwa na zahma kubwa na amesisitiza “hili lazima likome.” Amesema njaa si tishio tena bali janga la sasa, huku raia, wahudumu wa afya na waandishi wa habari wakiuawa wakati “macho ya dunia yakitazama.” Guterres ameikumbusha Israel wajibu wake wa kisheria kulinda raia na kuruhusu msaada wa kibinadamu bila vikwazo akisema “Hakuna visingizio tena. Hakuna vizuizi tena. Hakuna uongo tena,” akitoa wito wa usitishaji mapigano haraka na kuachiliwa kwa mateka wote.
- Kikosi cha 11 cha Tanzania TANZBATT 11 kinachohudumu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo DRC chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani MONUSCO kimetoa msaada wa magodoro kwa raia walioathirika na machafuko ya karibuni katika kijiji Oicha jimboni Kivu Kaskazini. Miongoni mwao ni Bi Masika Jistine na Mzee Bahati Paluku ambao hawakusita kuonesha furaha yao.
- Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili na hii leo Dkt Mwanahija Ali Juma, Katibu Mtendaji wa Baraza la Kiswahili, Zanzibar nchini Tanzania, BAKIZA anafafanua maana ya neno "MKWIJI!.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Audio Credit
Anold Kayanda
Sauti
9'59"