Afrika bado inaathirika kwa kiwango kikubwa, na kwa sasa inakumbwa na Ugaidi - Guterres
Wajumbe 15 wa Baraza la Usalama walikabidhiwa ripoti hiyo ya 21 ikimulika vitisho vinavyotokana na kikundi hicho ISIL ambacho kirefu chake ni Islamic State in Iraq and the Levant au pia Da’esh. Ingawa ripoti imegusia tishio la kikundi hicho katika maeneo mbalimbali duniani, mimi nitajikita zaidi barani Afrika!
Afrika bado inaathirika kwa kiwango kikubwa, na kwa sasa inakumbwa na shughuli kali zaidi za Da’esh kuliko eneo lingine duniani, ndivyo anavyosema Vladmir Voronkov, ambaye ni Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya kukabiliana na Ugaidi, UNOCT akihutubia Baraza la Usalama juu ya ripoti hiyo inayohusisha kipindi cha kuanzia Februari hadi Agosti mwaka huu.
Amegusia zaidi eneo la Afrika Magharibi akisema hali ya ugaidi katika eneo hilo pamoja na Ukanda wa Sahel ni ya dharura hivi sasa.
“Kipindi cha ripoti, kilishuhudia kuongezeka kwa shughuli za ISIL katika eneo la jangwa la Sahara, huku kikundi cha ISIL Afrika Magharibi kikijitokeza kama mtayarishaji mahiri wa propaganda za kigaidi na kuvutia wapiganaji wa kigeni wa kigaidi, hasa kutoka ndani ya eneo hilo.”
Mwakilishi wa Korea Kusini June-byoung Park yeye akamulika eneo la Afrika Mashariki akiangazia wapiganaji wa kigaidi wa kigeni au mamluki na Syria kutumia magereza yaliyofurika kusajili wapiganaji wa aina hiyo.
“Da’esh inaendelea kupanua vituo vyake vya kifedha na kiutendaji eneo la Afrika Mashariki, huku ikijinufaisha na hali ya ukosefu wa utulivu na wakati huo huo kueneza itikadi kali kwa wafungwa walio kwenye kambi kaskazini mashariki mwa Syria.”
Akawa na pendekezo:
“Hivyo basi, kuna uhitaji mkubwa kuliko wakati mwingine wowote wa kuwa na mpango wa kina kwa ajili ya wapiganaji wa kigaidi wa kigeni. Tunazisihi nchi zote husika kushirikiana kwa dhati ili kupata suluhisho linalokubalika kwa pande zote. Hatuwezi kuiruhusu Syria irejee kuwa kiini cha kulea ugaidi.”
Ripoti hiyo yenye kurasa 14 inaweka bayana kuwa Ahl al-Sunna wal-Jama‘a ambao ni tawi la Da’esh katika jimbo la Cabo Delgado nchini Msumbiji, lilikuwa na wapiganaji kati ya 300 hadi 400. Kikundi hicho kiliendelea kuwa na uimara, kikitekeleza mashambulizi ya mara kwa mara ya licha ya kwamba ni ya kiwango cha chini.
Kwa Somalia ambayo ni manusura wa vitendo vya kigaidi, safari bado ni mbali, kwa mujibu wa Naibu Mwakilishi wa taifa hilo la Pembe ya Afrika kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Mohamed Rabi A. Yusuf. Jawabu ni usaidizi wa kiufundi kwa nchi za Afrika, matumizi ya teknolojia kubaini mbinu za magaidi na kwamba,
“Njia ya mafanikio iko katika ushirikiano wa kimataifa wa kina, pamoja na nchi kumiliki mbinu za kukabili. Uzoefu wa Somalia ni ushahidi wa mbinu hii. Vita vyetu dhidi ya misimamo mikali ya kikatili vimeonesha kuwa suluhisho la kijeshi pekee halitoshi. Majibu madhubuti ni lazima yajumuishe nyanja za kisiasa, kiuchumi, na kiitikadi.”
Kaimu Mwakilishi wa Kudumu wa Sierra Leone kwenye Umoja wa Mataifa Balozi Kalilu Totangi ilipofika fursa ya kuwasilisha mchango wake, yeye hakumung’unya maneno akasema, “itikadi kali hustawi mahali ambapo kuna hali ya watu kutengwa, ukosefu wa ajira, na uongozi duni. Kuwekeza katika elimu, fursa za kiuchumi, na utawala shirikishi ni jambo la msingi. Hii ndiyo njia ya kuinyima Daesh/ISIL na washirika wake mazingira muafaka ya kuajiri wafuasi.”
Na kwa mantiki hiyo, Bwana Voronkov akatamatisha na mwelekeo wa ofisi yake akisema,
“Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kupambana na Ugaidi itaendelea kuweka kipaumbele katika kujengea uwezo, kubadilishana taarifa, na kutoa msaada maalum ili kusaidia nchi wanachama katika juhudi zao za kupambana na ugaidi.”
Tarehe 18 Agosti mwaka 2025 siku ya Jumatano, wajumbe 15 wa Baraza la Usalama walikutana kujadili Ripoti ya Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuhusu kikundi cha kigaidi cha ISIL/Da’esh.
Walikabidhiwa ripoti hiyo ya 21 ikimulika vitisho vinavyotokana na kikundi hicho ambacho kirefu chake ni Islamic State in Iraq and the Levant au pia Da’esh. Ripoti ikigusia tishio la kikundi hicho katika maeneo mbalimbali duniani, lakini makala hii initajikita zaidi barani Afrika!