Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

OHCHR: Israel isitishe mara moja mpango wa kulitwaa kijeshi eneo lote la Gaza

OHCHR: Israel isitishe mara moja mpango wa kulitwaa kijeshi eneo lote la Gaza

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo, ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mpango wa Serikali ya Israel  kutwaa kijeshi ukanda wote wa Gaza unaokaliwa kimabavu. 

Kupitia taarifa iliyotolewa kwa njia ya video leo Agosti 8 jijini Geneva, Uswisi, Msemaji wa Ofisi ya Haki za Binadamu ya Umoja wa Mataifa, OHCHR, Liz Throssell ameeleza kwamba, Kamishna wa haki za binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk anauona mpango huo wa Israel “unapingana na uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa ya Haki, ICJ kwamba Israel lazima ikomeshe uvamizi wake haraka iwezekanavyo, na unakwenda kinyume na utekelezaji wa suluhisho lililokubaliwa la mataifa mawili na pia haki ya Wapalestina ya kujitawala”. Anaendelea kueleza kwamba, “kwa ushahidi wote hadi sasa, hatua hii ya kuongeza uvamizi zaidi itasababisha kuongezeka kwa ufurushaji watu, mauaji zaidi, mateso yasiyovumilika, uharibifu usio na maana na uhalifu wa kikatili.”

Na kwa msingi huo, “vita vya Gaza lazima vikome sasa. Na Waisraeli na Wapalestina lazima waruhusiwe kuishi bega kwa bega kwa amani,” anasema Throssel kwa niaba ya Kamishna wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa akihitimisha kwamba, “badala ya kuongeza ukali wa vita hivi, Serikali ya Israel inapaswa kuelekeza juhudi zake zote katika kuokoa maisha ya raia wa Gaza kwa kuruhusu usambazaji kamili wa misaada usio na vizuizi, makundi yenye silaha ya Kipalestina yawaachie mara moja mateka bila masharti yoyote na. Wapalestina waliokamatwa kiholela na Israel pia wanapaswa kuachiwa mara moja na bila masharti yoyote.”

Pakua

Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa, Volker Türk, leo, ametoa wito wa kusitishwa mara moja kwa mpango wa Serikali ya Israel  kutwaa kijeshi ukanda wote wa Gaza unaokaliwa kimabavu. Anold Kayanda na maelezo zaidi.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
1'40"
Photo Credit
United Nations