Umoja wa Falme za Kiarabu wafanikisha vifaa vya matibabu ikiwemo damu kuwasili Gaza
Leo tuna habari njema kutoka Gaza, eneo la palestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel huko Mashariki ya Kati, Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na Umoja wa falme za Kiarabu UAE wamefanikiwa kuingiza dawa, vifaa tiba na damu salama kwa ajili ya matibabu ya wanagaza ambao wanaendelea kuteseka na madhila ya vita.
Kwa mujibu wa WHO tangu kuanza kwa mwezi huu wa Agosti wamefanikiwa kuingiza malori 36 za vifaa vya matibabu kama vile dawa za kusaidia wakati wa kufanya upasuaji, dawa ya kusaidia wanaougua kiwewe, dawa za matibabu yasiyo ya kuambukiza, vifaa vya maabara pamoja na vyakupima maji.
Lori moja limebeba makasha 11 ambayo yamefungwa vyema ili kutunza ubaridi, ndani ya makasha hayo kuna mamia ya mifuko ya damu salama, damu hii imeanza kusambazwa katika vituo mbalimbali vya afya ili kusaidia wenye uhitaji.
Akizungumza baada ya kupokea msaada huo, mratibu wa timu ya matibabu ya dharura kutoka WHO Heba Al Najjar amesema
“Dawa tulizonazo na vitu vilivyotolewa na UAE ni muhimu sana kwa wenye magonjwa sugu na watoto. Vinajumuisha sehemu muhimu ya mahitaji yetu ya kilasiku kwani nyingi za dawa hizi zinahitajika kwa kudumu, zikijumuisha baadhi ya antibiotics ambazo ni vigumu sana kupatikana.”
Afisa habari kutoka upande wa UAE Sharif Al-Neirab amesema misaada mingi zaidi ipo.
“Msafara huu ni sehemu ya msafara mkubwa wa misaada ya kimatibabu ulio njiani kuja Ukanda wa Gaza. Mungu akipenda, utawasili siku zijazo. Shehena ya malori tayari imeshafika kwenye maghala ya WHO, ambayo yataanza kusambaza dawa na vifaa tiba ambavyo vimewasili katika Ukanda wa Gaza, wakati huu ambapo wananchi wanakabiliwa na hali mbaya ya kiafya.”
WHO imehimiza uingizwaji huu wa misaada kuwa endelevu kwani dawa, vifaa tiba pamoja na bidhaa nyingine zinazoingizwa ni nyenzo muhimu katika utoaji wao wa huduma ya afya kwa wenye uhitaji.
Leo tuna habari njema kutoka Gaza, eneo la palestina linalokaliwa kwa mabavu na Israel huko Mashariki ya Kati, Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ulimwenguni WHO kwa kushirikiana na Umoja wa falme za Kiarabu UAE wamefanikiwa kuingiza dawa, vifaa tiba na damu salama kwa ajili ya matibabu ya wanagaza ambao wanaendelea kuteseka na madhila ya vita. Leah Mushi na taarifa zaidi.