Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kituo kipya cha kikanda cha SDGs Asia chazinduliwa Kazakhstan

Kituo kipya cha kikanda cha SDGs Asia chazinduliwa Kazakhstan

Umoja wa Mataifa na Kazakhstan wamesaini makubaliano ya Kazakhstan kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Umoja wa Mataifa cha Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa ajili ya ukanda wa Asia ya Kati na Afghanistan. 

Hafla ya utiaji saini makubaliano hayo ilifanyika jana Agosti 3 katika mji wa Almaty, mji mkubwa zaidi wa Kazakhsatan ikimhusisha Murat Nurtleu, Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Mambo ya Nje wa Kazakhstan na  Li Junhua, Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kwa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii, mbele ya mashahidi Kassym-Jomart Tokayev, Rais wa Kazakhstan, na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres.

Akizungumza baada ya hafla hiyo, Katibu Mkuu Guterres anasema,

“Kituo hiki kinawakilisha ufunguzi wa sura mpya kwa ajili ya eneo hili na kwa safari yetu ya pamoja kuelekea Malengo ya Maendeleo Endelevu. Kinatambulisha enzi mpya ya ushirikiano katika Asia ya Kati yenye misingi ya vipaumbele na suluhu za pamoja. Pia kina uwezo mkubwa wa kuonesha jinsi uhusiano imara kati ya viongozi wa eneo hili unavyoweza kutafsiriwa kuwa ujumuishaji wa kiuchumi zaidi, kwa manufaa ya watu wote. Hii ni muhimu zaidi kuliko wakati mwingine wowote.”

Guterres anaongeza kwamba kituo hiki kitakuwa maabara ya mawazo mapya,

“Hivi karibuni, kitafanya kazi kama kitovu cha ushirikiano wa kikanda, maabara ya mawazo na jukwaa la kuanzisha hatua. Kitawakutanisha serikali, timu za Umoja wa Mataifa katika nchi, mashirika ya kiraia, taasisi za elimu ya juu, sekta binafsi, mashirika ya kikanda, na taasisi za kifedha ili kuendeleza juhudi za pamoja, zinazoongozwa na nchi husika; na kukabiliana na changamoto kubwa za wakati wetu kutoka mabadiliko ya tabianchi na uhaba wa maji hadi ukosefu wa ajira kwa vijana, ukosefu wa usawa wa kijinsia na kutojumuishwa kidijitali.”

Anaongeza kwamba “kituo hiki kitafanya kazi na wadau kote katika ukanda huu na jamuiya ya kimataifa kusaidia njia ya Afghanistan kuelekea maendeleo endelevu  kwa kuheshimu kikamilifu haki za binadamu, zikiwemo haki za wanawake na wasichana, na kwa kuzingatia kujitegemea kiuchumi, amani na kueshimika.”

Katibu Mkuu akampongeza Rais Tokayev wa Kazakhstan kwa maono na uongozi wake katika kusaidia kuunda Asia ya Kati mpya ambayo itakuwa mhimili muhimu katika mfumo wa dunia.

Anasema, “Kazakhstan kwa upande wangu, ni ishara ya busara, mjenga madaraja na mjumbe wa amani. Ni jukwaa la watu wa makabila na dini tofauti kukutana na kutafuta hatima ya pamoja.”

Anahitimisha akikumbushia kuwa hatasahau kwamba Kazakhstan ilikataa silaha zake za nyuklia na ikawa, kutokana na mtazamo wao, ishara ya amani na unyang’anyaji silaha ambao ni muhimu leo kuliko wakati mwingine wowote.

Pakua

Umoja wa Mataifa na Kazakhstan wamesaini makubaliano ya Kazakhstan kuwa mwenyeji wa Kituo cha Kikanda cha Umoja wa Mataifa cha Malengo ya Maendeleo Endelevu kwa ajili ya ukanda wa Asia ya Kati na Afghanistan. Anold Kayanda anafafanua zaidi.

Audio Credit
Leah Mushi/Anold Kayanda
Audio Duration
3'10"
Photo Credit
UN in Kazakhstan