Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Kuinuka Pamoja: Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika Wakiongoza kwa Nguvu

Kuinuka Pamoja: Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika Wakiongoza kwa Nguvu

Siku ya kimataifa ya wanawake na wasichana wa asili ya kiafrika inalenga nini?

Leo, tarehe 25 Julai, ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika, ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu: “Kuinuka Pamoja: Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika Wakiongoza kwa Nguvu.” Idhaa ya Umoja wa Mataifa  imefanya mahojiano na Patricia Da Silva, Mratibu wa Kimataifa wa Timu ya Hakuna Kumwacha Yeyote Nyuma katika shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, UNFPA na kwanza akaulizwa afafanue kidogo siku hii inabeba nini hasa…

“Ni siku inayotambua kwa upekee mchango mkubwa wa wanawake wa asili ya Kiafrika katika jamii. Tunazungumzia sayansi, michezo, utamaduni, ujenzi wa jamii, kama wapambanaji na mengine mengi. Lakini pia, siku hii inatambua namna wanawake na wasichana wa asili ya Kiafrika wanavyoendelea kukumbwa na mzigo mara mbili wa ubaguzi wa rangi na jinsia. Na hili huwa na athari mbaya sana mara nyingine husababisha vifo kwa wanawake wa asili ya Kiafrika, familia zao na jamii kwa ujumla. Hivyo basi, hii ni siku ya kutafakari na kusherehekea bila shaka, lakini pia ni siku ya kutathmini tulipo na kwa nini tupo hapa.”

Akijibu kwa nini Siku hii ya kimataifa imetambuliwa rasmi mwaka jana tu na kwa nini imechukua muda mrefu kwa Umoja wa Mataifa kufanya hivyo? Patricia anasema,

“Naam, tazama, kubadilisha mifumo ya kimataifa kunaweza kuwa jambo linalochukua muda, kama tunavyojua sote. Nafikiri kwa sasa tunalenga zaidi kwamba angalau sasa tuna siku hii. Kitu tunachopaswa kuelekeza nguvu zetu kwacho ni kutambua uongozi wa wanawake wenye asili ya Kiafrika ambao kwa miongo mingi wamekuwa wakitetea umuhimu wa kutambua mchango wao. Na kwa kweli, wao ndio walio na maono, uelekeo huu wa harakati kutoka ngazi ya jamii ndio sababu ya sisi kuwepo hapa leo. Hivyo, tunapaswa kuelekeza nguvu zetu katika kusherehekea hilo kikamilifu. Kile tunachoshuhudia sasa, kwa kweli, si cha kushangaza ni taasisi zikiendelea kufuata nyayo za harakati za jamii ambazo zimekuwa zikiendelea kwa miongo mingi. Kwa hiyo, kutambuliwa kwa siku hii mwaka 2024 ilikuwa ni hatua muhimu sana na ya msingi. Na sasa tunafanya kazi kuhakikisha kwamba katika shughuli zetu, tunalenga katika kujumuisha usawa wa kijinsia na wa rangi katika jinsi tunavyofadhili, tunavyopanga, tunavyotekeleza na tunavyopima programu zetu za maendeleo ya kimataifa.”

Pakua

Leo, tarehe 25 Julai, ni Siku ya Kimataifa ya Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika, ikiwa na kaulimbiu ya mwaka huu: “Kuinuka Pamoja: Wanawake na Wasichana wa Asili ya Afrika Wakiongoza kwa Nguvu.” Idhaa ya Umoja wa Mataifa  imefanya mahojiano na Patricia Da Silva, Mratibu wa Kimataifa wa Timu ya Hakuna Kumwacha Yeyote Nyuma katika shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu, UNFPA na akafafanua kidogo siku hii inabeba nini hasa.

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
2'22"
Photo Credit
UNIC Mexico/Luis Arroyo