Trakoma au Vikope si tatizo tena la kiafya la umma nchini Burundi
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) leo Julai 11 limetangaza kwamba limeidhinisha Burundi kuwa imefanikiwa kuondoa ugonjwa wa macho unaofahamika kama trakoma au vikope kama tatizo la kiafya la umma, na kuifanya kuwa nchi ya nane katika Kanda ya Afrika ya WHO kufikia mafanikio haya muhimu.
Taarifa ya WHO iliyotolewa leo jijini Geneva, Uswisi na Bujumbura Burundi imeeleza kuwa ugonjwa huu wa Trakoma au Vikope ambao ni ugonjwa unaosababishwa na bakteria Chlamydia trachomatis na huenea kupitia mgusano wa moja kwa moja na watu, nyuso zenye uchafu au inzi waliogusa majimaji ya macho au pua ambapo maambukizi ya mara kwa mara husababisha makovu ndani ya macho, kope kuingia ndani ya jicho, na hatimaye upofu, duniani bado uko katika jamii zilizo pembezoni zaidi ambazo zina upungufu wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira na hivyo hatua hii ya Burundi ni kubwa.
Akizungumzia hatua hii waliyoifikia Burundi, Waziri wa nchi hiyo wa Afya ya Umma na Mapambano dhidi ya UKIMWI Daktari Lydwine Baradahana, amesema uthibitisho huu ni hatua kubwa katika dhamira yao ya usawa katika afya na kwamba ni ushindi wa pamoja uliowezekana kupitia zaidi ya miaka 20 ya kuhamasisha taifa na mshikamano wa kimataifa.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Daktari Tedros Adhanom Ghebreyesus amenukuliwa akisema, “kuondoa ugonjwa kama trakoma au vikope ni mafanikio makubwa ya afya ya umma yanayohitaji jitihada za muda mrefu na kujitolea.” Anaongeza kusema anaipongeza serikali na watu wa Burundi kwa kujitolea kwao na kwamba, “ni jambo la kufurahisha kuona Burundi ikijiunga na kundi la nchi zinazoongezeka ambazo zimeondoa angalau ugonjwa mmoja wa Magonjwa ya Kitropiki Yaliyopuunzwa, NTDs.”
Kwa sasa, kuna nchi 20 katika Kanda ya Afrika ya WHO zinazojulikana kuwa bado zinahitaji hatua za kuondoa ugonjwa huo wa macho wa trakoma au vikope na miongoni mwa hizo ni Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Kenya, Msumbiji, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda.
Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya Duniani (WHO) leo Julai 11 limetangaza kwamba limeidhinisha Burundi kuwa imefanikiwa kuondoa ugonjwa wa macho unaofahamika kama trakoma au vikope kama tatizo la kiafya la umma, na kuifanya kuwa nchi ya nane katika Kanda ya Afrika ya WHO kufikia mafanikio haya muhimu. Anold Kayanda anafafanua zaidi kuhusu taarifa hii.