Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

08 JULAI 2025

08 JULAI 2025

Pakua

Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayoturejesha katika mkutano wa 69 wa kamisheni ya hali ya wanawake duniani CSW69 kumsikia Mkurugenzi wa TEN/MET Nasra Kibukila kuhusu jitihada zao za kuhakikisha watoto wote wa Kitanzania wanapata elimu bora, jumuishi na yenye usawa, kwa kushirikiana na Serikali na wadau mbalimbali wa elimu ndani na nje ya nchi.

  1. Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa Volker Turk, amesikitishwa sana na mauaji ya jana ya watu wapatao 10, sambamba na uporaji na uharibifu wa mali wakati polisi walipokabiliana na waandamanaji kwenye mji mkuu wa Kenya, Nairobi na katika kaunti nyingine 16.
  2. Huko Geneva, Uswisi kumeanza mkutano wa siku 4 kuhusu matumizi ya Akili Mnemba au AI kwa maslahi ya wote ambapo Katibu Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la mawasiliano, ITU, Doreen Bogdan-Martin ameuliza washiriki ni jambo gani wanafanya AI ihudumie ubinadamu.?
  3. Na kuelekea kumbukizi yamauaji ya Srebrenica tarehe 11 mwezi huu wa julai, Umoja wa Mataifa unakumbuka mauaji hayo yaliyofanyika wakati wa vita vilivyofuatia baada ya kuvunjika kwa iliyokuwa Yugoslavia. Zaidi ya watu 100,000 huko Bosnia na Herzegovina waliuawa kati ya mwaka 1992 na 1995, wengi wao wakiwa waislamu wa Bosnia. Umoja wa Mataifa unasema mauaji ya Srebrenica ni moja ya vipindi vya kiza zaidi vya vita.
  4. Na katika mashinani tunakupeleka katika miji ya mpakani ya Matar na Muon katika eneo la Gambella nchini Ethiopia ambako maelfu ya wakimbizi wamewasili kutoka Jimbo la Upper Nile nchini Sudan Kusini wakikimbia vita na njaa, na sasa wanasubiri usajili na usaidizi kutoka kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la mpango wa chakula. Nyandow Wie Deng ni mmoja akisimulia yaliyomkumba.

Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!

Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
10'3"