03 JULAI 2025
Pakua
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayokupeleka nchini Uganda katika Mbuga ya Wanyama inayofahamika kwa jina Murchison Falls National Park kuangazia namna washiriki wa Kongamano la kimataifa la lugha ya Kiswahili lililofanyika mapema mwaka huu jijini Kampala walivyofurahia mazigira asili nchini Uganda na namna yanavyounufaisha ulimwengu.
- Mkutano wa 4 wa ufadhili kwa maendeleo umemalizika leo huko Sevilla, Hispania ambapo mashirika ya kiraia yametaka utekelezaji kwa vitendo kwa yale yaliyomo katika nyaraka iliyopitishwa iliyopatiwa jina Makubaliano ya Sevilla.Mmoja wa wawakilishi wa mashirika ya kiraia, Paula Sevilla amesema kinachohitajika ni uongozi kutoka nchi tajiri ambako ndiko zilizko kampuni kubwa zinazokwepa kodi.
- Ripoti mpya iliyotolewa leo na shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo, FAO kuhusu vijana na mifumo ya uzalishaij chakula na kilimo inaonesha kuwa karibu asilimia 85 ya vijana duniani wanaishi katika nchi za kipato cha chini na cha kati, ambako mifumo hiyo ni muhimu kwa ajira na maisha yao. Ripoti inasema kuwajumuisha vyema vijana katika mifumo hiyo kunaweza kuleta mchango wa hadi trilioni moja ya dola kwa uchumi wa dunia..
- Na mwezi uliopita wa Juni umeshuhudia ongezeko kubwa la familia za raia wa Afghanistan zikirejeshwa nyumbani kutoka Iran, tofauti na awali ambapo waliokuwa wakirejeshwa walikuwa ni wanaume peke yao.
- Na katika kujifunza lugha ya Kiswahili leo mchabuzi wetu Onni Sigalla, Mhariri Mwandamizi kutoka Baraza la Kiswahili la Taifa, BAKITA nchini Tanzania, anachambua neno KUTOHOA.
Mwenyeji wako ni Assumpta Massoi, karibu!
Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
9'58"