01 JULAI 2025
Pakua
Hii leo jaridani tunakuletea mada kwa kina inayotupeleka nchini Tanzania kumulika ukame na uhakika wa upatikanaji wa maji na kusikia jinsi taifa la Chile, linatumia sera kushawishi mabadiliko yanayoweza kukabiliana na tatizo hilo. Pia tunakuletea muhtasari na mashinani.
- Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Iran, Stefan Priesner amesema wanachofanya hivi sasa ni kupanga upya programu za Umoja wa Mataifa nchini humo wakimulika vipaumbele vipya kufuatia mashambulizi yaliyoanza tarehe 13 mwezi Juni mwaka huu na kubadili mwelekeo wa kazi zao. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geneva, Uswisi kutokea Tehran mji mkuu wa Iran, Bwana Priesner amesema sasa tuko kwenye mazugumzo ya serikali kuona ni vipi tutapanga upya programu zetu kukidhi mahitaji mapya yanayoanza kuwa dhahiri, ikiwa ni siku chache tu tangu mashambulizi yakome baada ya sitisho la mapigano kuridhiwa.
- Huko huko Geneva, Uswisi lakini akizungumza kutoka Nairobi Kenya, Shaun Hughes, ambaye ni Mratibu wa Dharura kwa mzozo wa Sudan katika shirika la Umoja wa MAtaifa la Mpango wa Chakula, WFP amewaambia waandishi wa habari kuwa hali ni tete kwa mamilioni ya raia wa Sudan waliokimbilia nchi jirani kuepuka mapigano nchini mwao.
- Shirika la Umoja wa Mataifa la masuala ya wanawake, UN Women linapotimiza miaka 15 tangu kuanzishwa kwake, limesema dunia imeshuhudia maendeleo muhimu katika usawa wa kijinsia ambayo yamebadilisha maisha ya wanawake na wasichana kote duniani. Licha ya ya kusherehekea, juhudi za kusukuma usawa wa kijinsia zinaonekana kurudi nyuma.
- Na mashinani, Mkutano wa 4 wa Ufadhili wa Maendeleo (FFD4) ukiendelea huko Sevilla Hispania, Natalia Toschi, Mkuu wa kitengo cha uwekezaji wa Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Maendeleo ya Kilimo, IFAD annasema ni wakati wa kufikiria upya jinsi maendeleo yanavyofadhiliwa kwa kuzingatia mifumo ya kilimo cha mazao ya chakula ili kukuza ukuaji wa kiuchumi vijijini.
Mwenyeji wako ni Anold Kayanda, karibu!
Audio Credit
Anold Kayanda
Audio Duration
9'59"