Guterres awaambia viongozi wa dunia huko Sevilla Ni wakati wa kufadhili mustakabali wetu na kubadilisha mwelekeo
Mkutano wa 4 wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo FFD4 umeng’oa nanga rasmi leo huko Selilla Hispania kwa wito wa kuziba pengo la ufadhili wa maendeleo ili kutimiza ahadi ya kimataifa ya kutomwacha yeyote nyumba. Mkutano huo uliowaleta pamoja washiriki 2,500 kutoka nchi 150 wakiwemo wakuu wa nhi 50 na wadau wengine unasema kuna pengo la dola trilioni 4 katika ufadhili wa maendeleo linalohitaji kuzibwa.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa António Guterres amewaambia viongozi wa dunia wanaokutana Sevilla, Hispania kuwa ni wakati wa “kufadhili mustakabali wetu na kubadilisha mwelekeo”. Akihutubia Mkutano huo wa 4 wa Ufadhili wa Maendeleo, Guterres amesema dunia imeingia wakati mgumu ambapo “maendeleo endelevu yanayochochewa na ushirikiano wa kimataifa sasa yanakumbana na vikwazo vikubwa.”
Guterres amesema pengo la ufadhili la dola trilioni 4 linaweka hatarini Ajenda ya 2030, huku akionya kuwa “ufadhili ndio injini ya maendeleo na kwa sasa injini hii inayumba.” Ametaka uwekezaji mkubwa na wa haraka ili kufikia malengo ya maendeleo endelevu, akisisitiza, “Tupo hapa Sevilla kubadilisha mwelekeo, kurekebisha na kuongeza kasi ya injini ya maendeleo.”
Akizungumzia maeneo ya hatua, Guterres amesema lazima rasilimali zitiririke, madeni yarekebishwe na mfumo wa kifedha wa dunia ubadilishwe. “Tunahitaji mfumo wa ushuru wa kimataifa ulio wa haki na unaoundwa na wote, si wachache pekee,” amesisitiza huku akiweka bayana kuwa mgogoro wa sasa wa gharama na maendeleo yaliyokwama ni “mgogoro wa watu unaowaacha watoto bila chanjo na familia bila chakula.”
Kwa upande wake, Mfalme Felipe wa Hispania amewaambia wajumbe, “ramani mpya ya mwelekeo lazima iwe dhahiri na inayotekelezeka,” huku Rais Pedro Sánchez wa nchi hiyo akiongeza, “Wakati wetu ni sasa na mahali petu ni hapa macho ya dunia yako kwenye ukumbi huu kuona tunachoweza kufanya pamoja.”
Katibu Mkuu wa mkutano huo Li Junhua anayesimamia Idara ya Masuala ya Uchumi na Kijamii ya Umoja wa Mataifa (DESA) naye ameahidi kuwa “Sevilla sio mwisho, bali ni jukwaa la kuzindua enzi mpya ya utekelezaji na mshikamano.”
Kutoka kwa viongozi wa taasisi za fedha duniani, wito umekuwa wazi, Ajay Banga Rais wa Benki ya Dunia amesema “kumaliza umaskini bado ni jukumu letu kuu,” huku WTO Shirika la Biashara Duniani ukisisitiza nchi maskini zisamehewe ushuru wa adhabu na na Shirika la Fedha Duniani IMF likitaka msingi mpana wa ushuru na suluhu endelevu za madeni.
Wote wametoa wito wa hatua za haraka ili kufanikisha kile Guterres alichokiita “uwekezaji katika mustakabali tunaotaka kuujenga pamoja.”
Mkutano wa 4 wa ufadhili kwa ajili ya maendeleo FFD4 umeng’oa nanga rasmi leo huko Selilla Hispania kwa wito wa kuziba pengo la ufadhili wa maendeleo ili kutimiza ahadi ya kimataifa ya kutomwacha yeyote nyumba. Mkutano huo uliowaleta pamoja washiriki 2,500 kutoka nchi 150 wakiwemo wakuu wa nhi 50 na wadau wengine unasema kuna pengo la dola trilioni 4 katika ufadhili wa maendeleo linalohitaji kuzibwa. Anold Kayanda amefuatilia na anatupasha zaidi