Muziki waunganisha jamii zilizogawanyika Malakal nchini Sudan Kusini
Katika juhudi za kuimarisha mshikamano na kurejesha matumaini miongoni mwa jamii zilizotengana kwa migogoro, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, hivi karibuni waliandaa tamasha maalum la muziki katika mji wa Malakal, jimbo la Upper Nile – eneo ambalo kwa miezi ya hivi karibuni limekuwa kitovu cha machafuko.
Tamasha hili lililokutanisha maelfu ya watu liliongozwa na msanii maarufu wa Sudan Kusini, Emmanuel Kembe, ambaye alitumbuiza wakazi kwa nyimbo zenye ujumbe wa amani na mshikamano.
Midundo ya muziki ilivyotawala anga iligeuka tiba kwa majeraha ya kijamii yaliyosababishwa na migogoro ya muda mrefu. Emmanuel anasema,
“Sisi ni taifa moja, na kile kinachodhuru watu wa Upper Nile, kinadhuru watu wote wa Sudan Kusini. Kama sehemu moja ya mwili inaumwa, sehemu nyingine pia huugua.”
Mkazi wa Malakal Neck Chol Deng aliyehudhuria tamasha hili anasema
“Ni jambo jema kuwa bado tuko Malakal, licha ya vita vilivyoikumba. Uharibifu ulikuwepo lakini bado tunaishi pamoja kama zamani. Malakal ni kitovu cha jimbo hili kinachowaunganisha watu wa Sudan Kusini na wale kutoka maeneo mengine; sote ni wasudan kusini.”
Viongozi waliohudhuria hawakusita kueleza dhamira yao ya kulinda amani na kuanzisha maendeleo ya kijamii na kiuchumi. Miongoni mwao ni Deng Joh Angok – Kaimu Gavana, Upper Nile anasema, “Serikali ina mpango thabiti kuhakikisha kila raia anaishi kwa uhuru, amani na katika mazingira salama. Tunafanya kazi ya kurejesha amani na kuanzisha maendeleo ili watu wapate amani ya kudumu na waishi tamaduni zao halisi. Tamaduni huhitaji usalama, na hilo ndilo jukumu letu.”
Katika juhudi za kuimarisha mshikamano na kurejesha matumaini miongoni mwa jamii zilizotengana kwa migogoro, ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Sudan Kusini, UNMISS, kwa kushirikiana na shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO, hivi karibuni waliandaa tamasha maalum la muziki katika mji wa Malakal, jimbo la Upper Nile – eneo ambalo kwa miezi ya hivi karibuni limekuwa kitovu cha machafuko. Sharon Jebichii anatupasha zaidi