Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Mapambano dhidi ya ndoa za kulazimishwa - Fatou Cissé

Mapambano dhidi ya ndoa za kulazimishwa - Fatou Cissé

Wakati ulimwengu ukiendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, tunaelekea nchini Mali, ambako Fatou Cissé, mkurugenzi wa filamu na mwanzilishi wa filamu iitwayo FURU, anatumia sanaa kuangazia suala zito la ndoa za kulazimishwa. Kupitia video maalum iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa, tunapata simulizi hiyo inayohusu wasichana wawili waliokumbwa na changamoto hizi. Fatou anawapa wasichana wa Kiafrika sauti na jukwaa la kuzungumza hadharani kuhusu dhuluma wanazokumbana nazo. 

Video hii imeanza na taswira ya mitaani katika moja ya vijiji huko nchini Mali, Magharibi mwa Afrika  na inamulika familia moja iliyojihusisha na ndoa ya kulazimishwa

Ni Fatou Cissé huyu, ambaye anaanza kueleza kwa ufupi kuhusu filamu ya FURU

FURU ni filamu ya wasichana wawili. Mmoja alipata ujauzito wa mpenzi wake ambaye hakuwa na uwezo wa kumuoa, hivyo wazazi wake waliona ndoa kama suluhisho ili kuepuka aibu kijijini. Baba yake alipata wazo la kumuozesha kwa rafiki yake.  Msichana mwingine ni huru na anajitegemea kwa kufanya kazi. Ananyanyaswa na vijana wa mtaa ambao wanataka aolewe kwa lazima kwa sababu ana umri wa kuolewa. Rafiki zake wa karibu wote tayari wameolewa hivyo jamii inaona huo ndio mkondo wa kawaida.”

Bi Fatou Cissé,akiwa manusura wa ndoa za kulazimishwa anazungumzia chanzo cha msukumo wake katika uandishi na utengenezaji wa filamu.

Nilipokuwa mdogo, nilipitia hali kama hiyo. Tulikuwa tunanyanyaswa na vijana wa mtaani. Wanakufuata barabarani, wanakudhalilisha. Hali hiyo ilinichosha sana. kupitia simulizi mbalimbali nilizosikia kutoka kwa wasichana wengine, ilinivutia kuandika na kutengeneza filamu hii, kwa sababu inanigusa mimi na wasichana wengi, hata sasa nchini Mali.”

FURU ilichaguliwa kushiriki katika Tamasha la Filamu la Afrika la New York na kuoneshwa kwa mara ya kwanza Amerika Kaskazini katika ukumbi wa kifahari wa Film at Lincoln Center. Kwa Fatou, hiyo ni hatua kubwa si tu kwa kazi yake ya sanaa, bali pia kwa ujumbe wenye uzito unaoubeba.

Nadhani ni jambo jema sana na ni nafasi ya pekee kwa filamu kuonekana hapa Marekani. Baba yangu ambaye alikuwa mmojawapo wa watengenezaji filamu mashuhuri zaidi barani Afrika aliniongoza kuingia katika sanaa kutokana na dhamira yake, ujasiri wake, na kupambana kwake bila kuchoka. Afrika tunasema hata kama hufanyi kile baba yako alifanya, jaribu kumwiga. Kwa hiyo mimi ninajaribu kufuata nyayo zake. Kupitia filamu kama FURU, ninatumaini kupaza na kuwakilisha sauti ya wasichana wasio na nafasi ya kusema. Ndoa za kulazimishwa ni unyanyasaji na ni wajibu wetu sote kupaza sauti na kupinga.”

Pakua

Wakati ulimwengu ukiendelea kupaza sauti dhidi ya vitendo vya ukatili wa kijinsia, tunaelekea nchini Mali, ambako Fatou Cissé, mkurugenzi wa filamu na mwanzilishi wa filamu iitwayo FURU, anatumia sanaa kuangazia suala zito la ndoa za kulazimishwa. Kupitia video maalum iliyoandaliwa na Umoja wa Mataifa, tunapata simulizi hiyo inayohusu wasichana wawili waliokumbwa na changamoto hizi. Fatou anawapa wasichana wa Kiafrika sauti na jukwaa la kuzungumza hadharani kuhusu dhuluma wanazokumbana nazo. Sharon Jebichii anasimulia.

Audio Credit
Selina Jerobon/Sharon Jebichii
Audio Duration
3'41"
Photo Credit
UN