Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

WHO: Mkutano wa 78 wa Baraza la Afaya Duniani umeng’oa nanga Geneva

WHO: Mkutano wa 78 wa Baraza la Afaya Duniani umeng’oa nanga Geneva

Wajumbe kutoka kote duniani wamekusanyika mjini Geneva, Uswisi, kwa ajili ya Mkutano wa 78 wa Baraza la Afya Duniani (WHA78) unaofanyika kuanzia leo Mei 19 hadi 27 Mei mwaka huu. Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Ulimwengu Mmoja kwa Afya” inaakisi dhamira ya pamoja ya kujenga mfumo wa afya wa kimataifa ulio imara, jumuishi na thabiti. Flora Nducha amefuatilia na hapa anatupasha zaidi

Kwa mujibu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa Duniani WHO katika Baraza hili “Nchi wanachama zitapitia mafanikio yaliyopatikana katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, ikiwemo utekelezaji wa Malengo ya “Triple Billion mkakati wa WHO unaolenga upatikanaji wa huduma za afya kwa wote, uimarishaji wa usalama wa kiafya na kuboresha ustawi wa watu”.

Ripoti hii pia inaashiria mwisho wa utekelezaji wa Mpango kazi wa 13 wa WHO au GPW13.

Katika ufunguzi wa Baraza hilo Mkurugenzi mkuu wa WHO Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus akizungumza kuhusu vipaumbele vya dunia na thamani isiyoelezeka ya afya na ambavyo sasa inawekwa rehani na ukata akisisitiza tofauti kubwa kati ya ufadhili wa afya na matumizi ya kijeshi au kibiashara.

“Inaonekana mtu fulani amebadilisha bei kwenye vitu ambavyo kwa kweli vina thamani katika dunia yetu.”
Ametahadharika kuhusu gharama ambayo dunia itaibeba kwa kutowekeza vya kutosha katika afya ya kimataifa na kukosoa vikali  bajeti zinazozingatia ulinzi wa kijeshi badala ya maandalizi dhidi ya magonjwa ya milipuko.

“Nchi zinatumia kiasi kikubwa cha fedha kujilinda dhidi ya mashambulizi kutoka kwa nchi nyingine, lakini hutumia kidogo sana kujilinda dhidi ya adui asiyeonekana ambaye anaweza kusababisha madhara makubwa zaidi.”

Pia ameweka bayana kwa nchi wanachama kuhusu uchaguzi ulio mbele yao kwa wito wito wa wazi kuchukua hatua na kuhakikisha ahadi zinaambatana na ufadhili

“Kama tukifikiri kuwa dola bilioni 2.1 kwa mwaka ni ndoto kubwa basi ni lazima aidha tupunguze matarajio yetu kuhusu WHO ni nini na inafanya nini, au tuongeze fedha. Najua ni lipi nitakalochagua, na natumaini nanyi mtachagua vivyo hivyo.”

Mkutano huu unatarajiwa kupitisha bajeti kamili ya kwanza kwa kipindi cha 2026–2027, chini ya Mpango Kazi wa 14 wa WHO (GPW14) mkakati mpya wa afya ya kimataifa kwa kipindi cha 2025 hadi 2028.

“Baraza hili ni hatua ya mabadiliko,” amesema , Dkt. Tedros  na kuongeza kuwa “Hatuangalii tu yaliyopita bali tunaunda mustakabali mpya wa afya ya dunia, tukizingatia usawa, utayari na uendelevu.”

Jambo jingine muhimu linalotarajiwa kujadiliwa katika Baraza hilo la Afya Duniani ni pendekezo la Mkataba wa maanga wa WHO ulioandaliwa na jopo la majadiliano la kiserikali kwa lengo la kuimarisha ushirikiano wa kimataifa na utayari wa kukabiliana na majanga ya kiafya yajayo.

Ukiidhinishwa, huu utakuwa mkataba wa kwanza ya aina yake tangu janga la coronavirus">COVID-19 kuibua mapungufu makubwa katika mifumo ya hatua ya dharura.

Dkt. Tedros amesisitiza kuwa “Mkataba huu ni ahadi yetu ya pamoja kuhakikisha haturudii tena kwa makosa ya zamani,”

Ajenda ya Baraza la 78 la Afya Duniani (WHA78) pia inajumuisha zaidi ya mambo 70 ya kiufundi na kiutawala, na wajumbe wanatarajiwa kuthibitisha ongezeko la michango ya lazima kutoka kwa nchi wanachama, kama sehemu ya juhudi za kuimarisha uhakika wa kifedha wa WHO.

Katika dunia inayokumbwa na changamoto nyingi za kiafya kuanzia majanga ya milipuko hadi athari za mabadiliko ya tabianchi  mkutano huu unawakilisha mshikamano wa kweli wa kimataifa chini ya mwamvuli wa kauli mbiu: “Ulimwengu Mmoja. Afya Moja”imesema WHO.

Pakua

Wajumbe kutoka kote duniani wamekusanyika mjini Geneva, Uswisi, kwa ajili ya Mkutano wa 78 wa Baraza la Afya Duniani (WHA78) unaofanyika kuanzia leo Mei 19 hadi 27 Mei mwaka huu. Kaulimbiu ya mkutano wa mwaka huu ni “Ulimwengu Mmoja kwa Afya” inaakisi dhamira ya pamoja ya kujenga mfumo wa afya wa kimataifa ulio imara, jumuishi na thabiti. Flora Nducha amefuatilia na hapa anatupasha zaidi

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'18"
Photo Credit
© WHO/Isaac Rudakubana