Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

Akina mama wakimbizi katika ukanda wa Gaza wanataabika bila huduma za afya

Akina mama wakimbizi katika ukanda wa Gaza wanataabika bila huduma za afya

Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, wanawake na wasichana wakiwemo wanawake wajawazito na wale waliojifungua, wamelazimika kukimbia makazi yao na wanaishi katika mazingira hatarishi bila huduma za msingi za kiafya. Sharon Jebichii anaangazia simulizi ya mama mmoja, mkazi wa kambi ya wakimbizi ya Jabalia, Kaskazini mwa Gaza, ambaye alijifungua akiwa amekimbia vita,na sasa anahangaika kumtunza binti yake mchanga.

Video ya Shirika la Umoja wa Mataifa la afya ya uzazi Idadi ya Watu Duniani (UNFPA)inamulika kambi ya Jabalia ikionesha akina mama wakitembea na watoto wao wachanga mmoja wao ni Nisma.

Nisma alilazimika kukimbia makazi yake akiwa mjamzito huku mashambulizi yakikithiri Kaskazini mwa Gaza. Safari ya kuyahama makazi yao ilikuwa ya mateso.Akiwa amembeba mwanaye mkononi anasema,

“Tulipolazimika kukimbia makazi yetu, tulitafuta hifadhi katika shule. Wakati huo nilikuwa mjamzito. Kwanza, tulilazilazimika kutembea kwa muda mrefu sana tukikimbia mgogoro huo. Nilikuwa na ujauzito wa miezi tisa na nilianza kuvuja damu sana. Nilipofika hapa, nilihisi kama nitakufa. Hali ilikuwa ngumu sana, sikuwa na mtu yeyote wa kunisaidia, nilikuwa peke yangu. Zaidi ya hayo, nilipata matatizo wakati wa kujifungua na ilibidi nifanyiwe upasuaji . Sijui ni nani aliyemchukua mtoto wangu. Nilikuwa nimechoka sana hadi nikapoteza fahamu.”

Hali si hali hata baada ya kufika kwenye kambi hiyo. Maisha kwa sasa bado ni ya kuhangaika, huku akikosa mahitaji ya msingi kwa ajili ya binti yake mchanga. Anasema,

Sina hata mahitaji yangu binafsi, hali ni mbaya zaidi kwa binti zangu. Binti mdogo hana maziwa wala nepi. Bei ya maziwa iko juu mno, hatuwezi kuimudu. Sasa ameanza kudhoofika kwa sababu ya utapiamlo.”

Msaada wa kibinadamu inahitajika kwa dharura ili kuokoa maisha ya wanawake na watoto katika Ukanda wa Gaza. UNFPA inalenga kuhakikisha huduma za afya ya uzazi na ulinzi zinapatikana.

Pakua

Huko Gaza, eneo la Palestina linalokaliwa na Israeli, wanawake na wasichana wakiwemo wanawake wajawazito na wale waliojifungua, wamelazimika kukimbia makazi yao na wanaishi katika mazingira hatarishi bila huduma za msingi za kiafya. Sharon Jebichii anaangazia simulizi ya mama mmoja, mkazi wa kambi ya wakimbizi ya Jabalia, Kaskazini mwa Gaza, ambaye alijifungua akiwa amekimbia vita,na sasa anahangaika kumtunza binti yake mchanga.

Audio Credit
Sharon Jebichii
Audio Duration
2'23"
Photo Credit
© UNFPA/Media Clinic