Chokoleti itengenezwayo Uganda yavuka mpaka na mabara -UNCTAD
Kutoka kakao ghafi huko Bundibugyo, magharibi mwa Uganda hadi Kampala mji mkuu wa kibiashara wa taifa hilo la Afrika Mashariki ndiko kunapatikana kiwanda cha kutengeneza chokoleti cha Equator kinachomilikiwa na Barbara Gonget na mume wake Gustav. Awali wazo la biashara hii lilionekana kutokuwa na mashiko. Ingawa hivyo baada ya ITC, ambacho ni Kituo cha Kimataifa ha Biashara kilicho chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD pamoja na wadau wao kuweka usaidizi wao, hali imebadilika na sasa biashara inavuka sio tu mipaka bali mabara. Wawili hao Kwa kuchanganya mbinu za hali ya juu, zinazojali jamii, na ufundi wa kitaalamu, wanabadili taswira ya uzalishaji wa chokoleti nchini humo.
Tuko nchini Uganda, na video ya Kituo cha Biashara duniani, ITC, kampuni tanzu ya shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD inatupeleka moja kwa moja kwenye kiwanda cha kutengeneza chokoleti cha kampuni ya Equator Chocolate.
Na umsikiaye ni Barbara Gonget, mjasiriamali na Mkurugenzi wa Equator Chocolate, akielezea usuli wa biashara hii. “Wakati mume wangu alipopata wazo la kuanzisha utengenezaji wa chokoleti nchini Uganda, kwa kweli sikudhania kuwa itawezekana. Nilifikiri kuwa chokoleti zinatengenezwa sana sana Ulaya, na hivyo ndio nimefahamu tangu ninakua. »
Wafanyakazi wamevalia makoti, kofia na barakoa, vyote rangi nyeupe na wanaokana wakipanga chokoleti ambazo zimeshakamilika tayari kufungashwa. Pembeni ni bakuli lenye rojo la chokoleti. Bi. Gonget anasimulia safari nzima ya biashara hii.“Safari yetu haijawa rahisi. Tulianza kwa kununua kakao kwa wingi. Tulinunua kutoka kwa mkulima yeyote yule na wakati huo hatukufahamu kuhusu ubora. Kwa hiyo mwanzoni chokoleti zetu hazikuwa na kiwango cha ubora kama ilivyo hivi sasa.”
ITC ndio iliwafungua macho kupitia mradi wa MARKUP unaofadhiliwa kwa pamoja na Muungano wa Ulaya na Jumuiya ya Afrika Mashariki, EAC.“Tulipata wataalamu kutoka ITC ambao walifika hapa na kutupatia mafunzo sisi pamoja na wakulima kuhusu taratibu bora na sahihi za uchachushaji wa kakao. Tunapata kakao kutoka Bundibugyo, ambayo iko magharibi kabisa mwa Uganda. Tunasafirisha hadi hapa.”
Huko Bundibugyo wanashirikiana na wakulima zaidi ya 70 walio katika vyama mbalimbali vya ushirika. Ingawa hivyo familia zaidi ya 700 zinanufaika na kampuni hii kupitia ununuzi wa kakao yao. Kakao inasafirishwa kwenye magunia hadi Kampala kiliko kiwanda hiki.“Kakao inaletwa hapa kiwandani kwetu kwa ajili ya kutengeneza chokoleti. Kisha zinawekwa hapa hadi mchakato wa kukaanga unakamilika. Na baada ya hapo ni awamu hii ambayo unaona timu hii inafanya hivi sasa.”
Bi. Gonget anaelezea kile kinachofanyika baada ya kukaanga kakao“Kakao zinakaangwa, kisha zinamenywa kwa mikono na kutolewa Maganda. Baada ya hatua hiyo kukamilika hapa, mbegu zinasagwa na tunatoa siagi ya kakao. Kisha chokoleti hupikwa na kufunikwa juu ya karanga. Baadaye, huwekwa kwenye jokofu na kisha kufungashwa.”
Anatuonesha chokoleti ilivofungwa vizuri ikipatiwa jina Rafiki na iko tayari kusafirishwa kwenye Denmark kwa ajili ya kuuzwa. Na nyingine zimefungashwa kwenye makaratasi yenye nembo ya Muungano wa Ulaya, EU.“Kila kitu kinatengenezwa hapa. Makasha ya kufungua, chokoleti – hivyo basi tunatuma bidhaa iliyokamilika. Kama tunavyoweza kuona pia, Muungano wa Ulaya wamekubali wazo hili. Tuna chokoleti zetu humo. Kwa kuchakata kakao hizi zenye ubora wa hali ya juu, tumeweza kutengeneza chokoleti bora sana yenye ladha nzuri, na inayoweza kushindana na viwango vya kimataifa.”
Pamoja na Denmark, wana ubia pian a mataifa mengine.“Tumeingia ubia na kampuni moja huko Congo ambayo inanunua kiasi kikubwa cha chokoleti yetu hadi sasa. Sasa tunapanua biashara yetu hadi Kenya, na hivi karibuni tutakuwa Rwanda na katika nchi mbalimbali jirani. Kwa hiyo, ndiyo, ningesema kwamba soko la kikanda na la kuuza nje ni maeneo ambayo tunataka kuyazingatia kwa dhati, na kujaribu kupata uwiano mzuri kati ya yote mawili pale tunapoweza.”
Kutoka kakao ghafi huko Bundibugyo, magharibi mwa Uganda hadi Kampala mji mkuu wa kibiashara wa taifa hilo la Afrika Mashariki ndiko kunapatikana kiwanda cha kutengeneza chokoleti cha Equator kinachomilikiwa na Barbara Gonget na mume wake Gustav. Awali wazo la biashara hii lilionekana kutokuwa na mashiko. Ingawa hivyo baada ya ITC, ambacho ni Kituo cha Kimataifa ha Biashara kilicho chini ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo, UNCTAD pamoja na wadau wao kuweka usaidizi wao, hali imebadilika na sasa biashara inavuka sio tu mipaka bali mabara. Wawili hao Kwa kuchanganya mbinu za hali ya juu, zinazojali jamii, na ufundi wa kitaalamu, wanabadili taswira ya uzalishaji wa chokoleti nchini humo.Je wamefanya nini? Assumpta Massoi anafafanua zaidi kwenye makala hii iliyofanikishwa na ITC.