Stadi za kuoka mikate zaleta furaha kwa mkimbizi Thérèse huko Beni nchini DRC
Jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Thérèse Kavira, mwanamke shupavu aliyelazimika kukimbilia mji wa Beni baada ya waasi kuvamia kijiji chake sasa ameona nusu kwenye maisha yake kufuatia mafunzo ya kuoka mikate yaliyotolewa na ofisi ya Utafiti na Usaidizi kwa Mahusiano ya Kimataifa nchini humo pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO na sasa anajikimu kimaisha.
Machafuko mashariki mwa DRC yalimlazimu Thérèse na familia yake kukimbia hadi Eringeti kitongoji kilichoko mji wa Oicha jimboni Kivu Kaskazini.
“Tulipofika Eringeti, tuligundua kuwa maisha yalikuwa magumu na changamoto zilikuwa nyingi. Kutokana na hali hiyo, tulilazimika kuondoka na kuelekea Beni kwa matumaini ya kupata nafuu. Tulipowasili Beni, tuliandikishwa kama wakimbizi. Siku moja, baada ya kusajiliwa, tulisikia tangazo kutoka MONUSCO, kuwa wale waliokuwa na nia ya kujifunza kazi za mikono wangepata msaada. Maneno hayo yalinigusa, nami nikaamua kuchukua hatua.”
Thérèse alipata nafasi ya kipekee kupitia MONUSCO, ambapo video ya MONUSCO iliyochapishwa kwenye mtandao wa X inaonesha yeye na wenzake wakioka mikate na bidhaa nyingine za unga wa ngano.
Stadi hizo zimemwezesha kujitegemea, maisha yake yamebadilika kwa kiasi kikubwa, na anajivunia kuwa na uwezo wa kuhudumia familia yake bila kutegemea msaada wa nje, na kwa furaha anasema,
"Kwangu mimi, nafurahi sana kwa sababu maisha yangu yameboreshwa. Sitakuwa nakosa kitu tena. Watoto wangu hawatalala njaa, watapata masomo bora, na nitaweza kuwalipia karo yao. Sitalia tena."
Jimboni Kivu Kaskazini, Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, Thérèse Kavira, mwanamke shupavu aliyelazimika kukimbilia mji wa Beni baada ya waasi kuvamia kijiji chake sasa ameona nusu kwenye maisha yake kufuatia mafunzo ya kuoka mikate yaliyotolewa na ofisi ya Utafiti na Usaidizi kwa Mahusiano ya Kimataifa nchini humo pamoja na ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani DRC, MONUSCO na sasa anajikimu kimaisha. Sharon jebichii na taarifa zaidi.