26 MACHI 2025
Hii leo jaridani tunaangazia janga la njaa katika ukanda wa Gaza, na hali ya wakimbizi wa DRC waliokimbilia Burundi kufuatia machafuko. Makala tunakwenda nchini Chad na amshinani nchini Sudan, kulikoni?
- Watu zaidi ya milioni 1 wako katika hatari ya kukosa chakula endapo misaada haitoruhusiwa kuingia Gaza wakati huu mashambulizi makali ya Israel yakizidisha janga la kibinadamu yameonya leo mashirika ya misaada ya Umoja wa Mataifa.
- Hali ya kibinadamu ya wakimbizi zaidi ya 100,000 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC, waliokimbilia nchini Burundi kusaka usalama kutokana na mapigano mashariki mwa nchi yao katika katika kipindi cha chini ya miezi mitatu, iliyopita ni ya mashaka, wakati huu ambapo ufadhili unazidi kukumbwa na mkwamo, wakikabiliwa na uhaba wa huduma kama chakula, huku kukiwa na pengo la ufadhili. Je ni madhila yapi? Sharon Jebichii anafafanua zaidi kupitia video iliyoandaliwa na shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi,UNHCR.
- Makala ambapo Assumpta Massoi anamulika harakati za wanakikundi wanawake wasiojua kusoma na kuandika huko Chad za kuepusha zahma hiyo isikumbe watoto wao wa kike.
- Na katika mashinani fursa ni yake Bi. Argentina Matavel Piccin, Mwakilishi wa muda wa shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu Duniani UNFPA nchini Sudan, ambaye kupitia mahojiano na UN News, amesema hali ya wanawake na wasichana nchini Sudan ni ya kuhuzunisha kufuatia vita inayoendelea.
Mwenyeji wako ni Leah Mushi, karibu!