Mtazamo wa Kimataifa Habari za kiutu

UNAIDS: Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani ni janga kubwa kwa vita dhidi ya ukimwi na chachu ya vifo

UNAIDS: Kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani ni janga kubwa kwa vita dhidi ya ukimwi na chachu ya vifo

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS leo limeonya kwamba kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani sio tu janga kwa vita dhidi ya gonjwa hilo bali ni chachu ya vifo na ongezeko la maambukizi mapya. Flora Nducha amefuatilia onyo hilo lililotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Mkurugenzi mtendaji wa UNAUDS Winnie Byanyima alipozungumza na waandishi wa habari. 

Bi. Byanyima amewaambia waandishi wa habari kwamba serikali ya Marekani imekuwa mfadhili mkubwa wa mipango ya kukabiliana na UKIMWI, hasa kupitia Mpango wa Dharura wa Rais wa Marekani wa Kupambana na UKIMWI (PEPFAR).

Hata hivyo, kukatwa kwa msaada wa kifedha sasa kunahatarisha programu muhimu zinazotoa matibabu ya kuokoa maisha, huduma za kuzuia maambukizi, na utafiti wa kisayansi hasa kwa nchi ambazo msaada huo ni tegemeo kubwa mathalani amesema “Lakini sasa hebu fikiria nchi kama Tanzania ambayo inategemea asilimia 94 ya mapambano yake msaada kutoka nje na hasa Marekani hivyo athari zitakazojitokeza unaweza kuona .”

UNAIDS inatahadharisha kuwa bila msaada wa kifedha wa kutosha, mamilioni ya watu, hasa katika nchi zenye kipato cha chini, wanaweza kukosa huduma muhimu za UKIMWI na hasa wale wanaotegemea dawa za kupunguza makali ya ugonjwa huo ili kuendelea kuishi akisema “Hata kufurugwa kwa muda mfupi kwa matibabu kuna athari kubwa kwa watu wanaoishi na HIV. Endapo mtu ataruka kunywa dozi kutamsababishia usugu wa dawa , hii itaongeza idadi ya virusi, na hii itaongeza maambukizi.”

Bi Winnie amesema waathirika wakubwa katika zahma hii ya ukataji ufadhili ni jamii zilizo hatarini, zikiwemo wanawake, watoto, na makundi yaliyotengwa ambayo tayari yanakumbwa na changamoto za kupata huduma za afya hususan  Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ambako kiwango cha maambukizi ya UKIMWI bado ni cha juu, na hivyo kupungua kwa msaada wa kifedha kunaweza kufuta mafanikio yaliyopatikana katika kupunguza maambukizi na kuboresha upatikanaji wa matibabu.

Ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka ili kuzuia kurudi nyuma kwa maendeleo katika juhudi za kimataifa za kumaliza janga la UKIMWI ifikapo 2030.

UNAIDS na mashirika mengine ya afya duniani yameitaka serikali ya Marekani kufikiria upya uamuzi wake wa kupunguza ufadhili, yakisisitiza kuwa uwekezaji endelevu ni muhimu ili kuendelea kupiga hatua katika mapambano dhidi ya UKIMWI.

Pakua

Shirika la Umoja wa Mataifa la kupambana na ukimwi UNAIDS leo limeonya kwamba kusitishwa kwa ufadhili wa Marekani sio tu janga kwa vita dhidi ya gonjwa hilo bali ni chachu ya vifo na ongezeko la maambukizi mapya. Flora Nducha amefuatilia onyo hilo lililotolewa leo mjini Geneva Uswisi na Mkurugenzi mtendaji wa UNAUDS Winnie Byanyima alipozungumza na waandishi wa habari.

Audio Credit
Flora Nducha
Audio Duration
2'44"
Photo Credit
© UNAIDS/Cynthia R Matonhodze